Hatua ya mwisho ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya
26 Mei 2019Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa katika mataifa 21 Jumapili (26.05.2019), ikiwa ni pamoja na mataifa makubwa ya Umoja wa Ulaya ya Ujerumani, Ufaransa, Italia, Uhispania na Poland.
Mataifa haya matano kwa pamoja yanatoa karibu nusu ya wabunge wa Umoja wa Ulaya katika bunge hilo,348 kutoka idadi ya wabunge 751.
Upigaji kura katika bunge pekee la kimataifa duniani ulianza siku ya Alhamis ambapo Uholanzi na Uingereza zilianza kupiga kura , na kisha kufuatiwa na Ireland na Jamhuri ya Cheki siku ya Ijumaa na Latvia, Malta na Slovakia siku ya Jumamosi.
Jumla ya raia milioni 420 wanahaki ya kupiga kura . Watafiti wa uchaguzi wanatarajia kiwango cha chini cha wapiga kura katika uchaguzi wa hapo awali mwaka 2014, ambao ilikuwa ni asilimia 43 tu, inaweza kupanda kidogo mara hii.
Vyama vikubwa vya kisiasa katika Umoja wa Ulaya vimesema uchaguzi wa mwaka huu unaweza kuwa uchaguzi wa mabdiliko katika maisha.
Wagombea wakuu katika chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha European Peoples Party EPP, Manfred Weber wa Ujerumani, na mgombea wa chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto kwa upande wa wasoshalisti barani Ulaya, Frans Timmermans, PES, makamu wa rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya anayeondoka madarakani kutoka Uholanzi, wote wanakubaliana kuhusiana na maelezo haya wakati wa kampeni za uchaguzi.
Ulinzi wa maadili ya kidemokrasia
Wasi wasi wao mkubwa katika uchaguzi huu ni kuendelea na hali ya umoja katika Umoja wa Ulaya, kulinda demokrasia ya "kiliberali" utaratibu unaooungwa mkono na vyama vya sisa za kizalendo miongoni mwa waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban.
Mwanasiasa wa Italia mfuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia Matteo Salvini , kwa upande wake, anataka kupunguza kwa kiasi kikubwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya.
Kama walivyo wafuasi wa siasa za kizalendo katika mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya, Salvini anafuata kauli mbiu ya "Nchi yangu kwanza" chama chake huenda kikawa nguvu ya ushawishi nchini Italia katika uchaguzi huu.
Wiki ya mwisho ya kuelekea katika uchaguzi huu bila shaka haikukosa vituko. Nchini Austria, muungano wa kihafidhina unaounda serikali uliporomoka baada ya mwanachama wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Freedom Party, kiongozi wa zamani Heinz-Christian Strache, alionekana katika vidio akionekana kutoa kandarasi ya serikali kwa mpwa wa tajiri mkubwa wa Urusi ili kuweza kupata msaada wa kampeni.
Wachunguzi wa uchaguzi bado wana shaka iwapo kashfa hii itakuwa na athari yoyote katika uchaguzi wa Umoja wa Ulaya.
Davide Ferrari , wa taasisi ya utafiti ya Votewatch mjini Brussels, ameiambia DW kwamba athari zitakuwa ndogo kwa Austria. Wapiga kura wa siasa kali za kizalendo hawajali kabisa kuhusu maadili. Kwa wao ni kuhusiana na upinzani tu," amesema.
Mwandishi: Bernd Riegert / Brussels / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Yusra Buwayhid