Hatua za kulipizana kisasi kati ya Malaysia Korea Kaskazini
7 Machi 2017Hatua hiyo inatokana na mzozo juu ya kuuwawa kwa kaka wa baba mmoja wa rais wa Korea Kaskazini mauaji ambayo yametokea nchini Malaysia.
Hatua hiyo ya serikali ya Korea Kaskazini isio ya kawaida imekuja Jumanne (07.03.2017) wakati nchi hiyo ikikabiliwa na ongezeko la shinikizo la kimataifa kutokana na mfululizo wa makombora ilioyafyatuwa katika bahari ya Japani kwa kukaidi vikwazo vikali vya kimataifa vyenye kukusudia kukomesha mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia. wa nchi hiyo.
Matukio hayo ya leo yanayonyesha kuzidi kupamba moto kwa mvutano wa nchi hiyo na Malaysia ikiwa ni wiki tatu baada ya ndugu wa baba mmoja wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jon-Un kuwawa katika uwanja wa ndege wa Malaysia kutokana na sumu inayouwa mishipa ya fahamu ya VX iliopigwa marufuku.
Korea Kaskazini imeamuwa kuwapiga marufuku kwa muda kuondoka nchini humo raia wa Malaysia hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la serikali KCNA likikariri wizara ya mambo ya nchi za nje ya nchi hiyo
ikisema marufuku hiyo itaendelea kubakia hadi pale usalama wa wanadiplomasia na raia wake walioko Malaysia utapokuwa umehakikishwa kwa suluhisho la haki la tukio hilo lililotokea Malaysia.
Wizara ya mambo ya nje ya Malaysia imesema raia wake 11 hivi sasa wako nchini Korea Kaskazini wakiwemo wafanyakazi watatu wa ubalozi ,wanafamilia sita na wengine wawili wanaofanya kazi katika shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa.
Razak alaani kuzuiliwa kwa raia wao
Waziri Mkuu wa Malaysia Najib Razak amelaani marufuku hiyo na kuamuru marufuku kama hiyo kwa nyendo za raia wote wa Korea Kaskazini walioko nchini Malaysia ambapo wachambuzi wanasema wanaweza kufikia 1,000.
Razak amesema "Kuwalinda raia wetu ni kipau mbele changu cha kwanza na hatutosita kuchukuwa hatua zote zinazohitajika iwapo wakiwa katika tishio.Natowa wito kwa uongozi wa Korea Kaskazni kuwaruhusu mara moja raia wetu kuondoka nchini humo ili kuepusha kuendelea zaidi kwa mvutano."
Najib amesema kitendo hicho cha kuchukiza kuwashikilia mateka moja kwa moja raia wao ni kudharau kabisa sheria ya kimataifa na kanuni za kidiplomasia.Ameongeza kusema kwamba likiwa kama taifa la amani Malaysia imejitolea kudumisha ushirikiano wa kirafiki na nchi zote .
Korea Kusini imeilaumu serikali ya Korea Kaskazini kwa mauaji ya kaka wa baba mmoja wa kiongozi wa nchi hiyo na serikali ya Malaysia imekuwa ikitaka kuwahoji Wakorea Kaskazini kadhaa ambapo polisi wa nchi hiyo imewataja wanane wanaotafutwa kwa kuhusishwa na mauaji hayo akiwemo mwanadiplomasia mwandamizi wa nchi hiyo na mfanyakazi wa shirika la ndege la taifa wawili kati ya haó watatu inaaminika wamejificha katika ubalozi wa nchi hiyo nchini Malaysia.Hadi sasa watu wawili tu wamefunguliwa mashtaka mwanamke wa Kivietnam na mwanamke wa Indonesia.
Wakati hayo yakijiri Marekani imeanza kuweka vifaa vya kwanza vya mfumo wake wa makombora nchini Korea Kusini baada ya Korea Kaskazini kufanya majiribio manne ya makombora ya masafa marefu.Hatua hiyo ya Marekani imeikasirisha China.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters /AFP
Mhariri :Yusuf Saumu