Hatua za kuwaondoa raia Aleppo zakwama
17 Desemba 2016Francois Delattre aliwaambia waandishi habari nje ya ukumbi wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba nchi yake na Ujerumani zimeomba kikao hicho cha jana Ijumaa. Amesema kuwa iwapo makubaliano hayatapatikana kuhusiana na usalama wa kuwaondoa raia na kuwezesha misaada ya kiutu kuingia katika mji huo uliozingirwa kwa uangalizi wa wachunguzi wa kimataifa, Ufaransa na washirika wake wanaweza kuitisha kikao maalum cha dharura cha wanachama 193 wa baraza kuu la Umoja wa mataifa.
Delattre amesema Ufaransa tayari imeanza kutayarisha mswada kwa ajili ya kufikishwa katika baraza la Usalama.
Uondoaji watu kutoka Aleppo mashariki umefikisha mwisho ngome kuu na muhimu ya waasi nchini Syria na kuwa wakati muhimu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, ambavyo vimefikisha miaka sita sasa.
Juhudi za kuwaondoa raia usiku zilikwama baada ya kuzuka kwa mapambano ya silaha na kusababisha hofu kwamba hatua za amani za kusalimu amri kwa wapinzani katika eneo hilo kunaweza kushindwa wakati maelfu ya watu wanaaminika kuwa bado wako katika eneo hilo.
Delattre amesema kikao hicho cha baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kitajumuisha barua ya mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien. "Tunaendelea kupata taarifa za kukanganya juu ya kile hasa kinachotokea katika eneo hilo," amesema.
Majadiliano ya kitaifa
Urusi ni mshirika muhimu wa rais Bashar al-Assad katika vita vyake na makundi ya upinzani ya wasi. Balozi wa Urusi katika Umoja wa mataifa Vitaly Churkin , amesema jukumu muhimu la haraka nchini Syria hivi sasa ni kumaliza shughuli zote za kijeshi na kuanza majadiliano kati ya serikali na upinzani.
Churkin aliliambia baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa kwamba "Syria imethibitisha zaidi ya mara moja kuwapo kwake tayari kushiriki katika majadiliano haya."
Waziri wa mambo ya kigeni wa New Zealand Murray McCully aliliambai baraza la Usalama kabla ya kuanza kikao cha faragha kuhusu Aleppo kwamba baraza hilo halijaweza hadi sasa kutimiza majukumu yake ya kuwaondoa raia na kutoa msaada wa kiutu katika mji huo.
"Hadi pale hali hiyo itakapobadilika, mawazo yetu ni kwamba kikao maalum cha dharura cha baraza kuu la Umoja wa mataifa ni hatua nyingine sahihi," amesema.
Katibu mkuu anasikitika
Katibu mkuu anayeondoka madarakani Ban Ki-moon amesema Umoja wa mataifa uko tayari kutoa msaada kuwaokoa watu wengi kadri inavyowezekana - hata ikiwa operesheni iliyofanyika usiku imesitishwa.
Akizungumza na waandishi habari katika kikao chake cha mwisho na waandishi habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jana Ijumaa, Ban aliita vita nchini Syria " vinavyonivunja moyo."
Hata hivyo amesema maelfu ya watu wameondolewa kutoka Aleppo mashariki usiku kwa msaada wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, shirika la msalaba mwekundu na hilali nyekundu, ikiwa ni pamoja na wagonjwa 194 ambao waliondolewa na kupelekwa hospitalini katika maeneo mengine ya Syria na Uturuki.
"Nasikitika sana kwamba tunalazimika kusitisha operesheni hii katika wakati huu," alisema katika mkuu Ban.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Bruce Amani