1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatumbadilishi Loew yasema DFB

12 Septemba 2016

Shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB linataka kocha wa timu ya taifa Joachim Loew kuendelea baada ya fainali za kombe la dunia la mwaka 2018 lakini halitamhimiza kuamua haraka kabla ya mashindano hayo nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/1K0ns
UEFA EURO 2016 Deutschland - Ukraine Nationaltrainer Joachim Löw
Kocha wa Ujerumani Joachim LoewPicha: picture-alliance/GES/Marvin Guengoer

Rais wa DFB Reinhard Grindel aliliambia jarida la michezo la Kicker la leo Jumatatu kwamba kocha huyo aliyeipatia ubingwa wa dunia Ujerumani mwaka 2014 ana haki ya kuamua binafsi wakati gani anataka kurefusha makubaliano yake, iwapo anataka.

"Kwa heshima ya kocha wetu bingwa wa dunia Jogi anapaswa kuamua binafsi. Iwapo anataka kufanya uamuzi mara tu baada ya fainali za kombe la dunia nitasema tufanye hivyo," alisema Grindel.

Loew alisema wakati wa ufunguzi wa michuano ya mchujo ya kombe la dunia, kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Norway Septemba 4 , kwamba kwa sasa hafikirii juu ya hali ya mkataba wake.

Deutschland DFB neuer Präsident Reinhard Grindel (kushoto)
Rais wa shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB Reinhard GrindelPicha: Getty Images/AFP/D. Roland

Loew mwenye umri wa miaka 54, alianza kuifunza timu ya taifa ya Ujerumani mwaka 2006 baada ya kuwa chini ya Juergen Klinsmann kwa miaka miwili. Alirefusha mkataba wake baada ya fainali za kombe la dunia mwaka 2010 na kufuatiwa na kurefusha tena kabla ya mashindano makubwa.

Grindel alisema DFB inataka kuendelea kufanyakazi na Loew kama kocha kwa muda mrefu na hajafikiria kumbadilisha.

"Nina ahusiano mazuri na Jogi Loew. Kila wakati niko tayari kwa mazungumzo iwapo anataka kuzungumzia juu ya hali yake ya baadaye," alisema Grindel.