Hatutaki silaha za Nuklia yasema Iran
30 Agosti 2012Iran iliyowakaribisha wajumbe wa nchi 120 wanachama wa Jumuiya hiyo wakiwemo karibu viongozi wakuu 30,wa Kundi lisilokuwa na mafungamano na upande wowote inatazamia kuuthibitishia ulimwengu kwamba juhudi za nchi za Magharibi za kuitenga na kuiadhibu kiuchumi kutokana na mpango wake wa Nuklia,ni hatua zilizoshindwa.
Mtazamo huo umesisitizwa katika ufunguzi wa mkutano huo mapema asubuhi ya leo katika hotuba ya kiongozi wa juu kabisa wa taifa hilo la Kiislamu Ayatollah Ali Khamenei,aliyesema kwamba kauli mbiu ya Iran ni kusonga mbele na mpango wa kuwa na nishati ya Nuklia kwa ajili ya wananchi wake na sio kwa ajili ya silaha.
Upande mwingine katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon anayehudhuria mkutano huo ameitaka Iran kuuthibitishia ulimwengu kwamba mpango wake huo wa Nuklia ni wa amani pia ameikosoa nchi hiyo kwa kauli zake za kupinga mauaji ya kinyama dhidi ya wayahudi ya Holocoust pamoja na kupinga haki ya kuweko taifa la Israel.
Kwa mujibu wa naibu msemaji wa Katibu mkuu Farhan Haq,Ban Ki Moon yuko kwenye mkutano huo kwa lengo la kushirikiana na wanachama wa Jumuiya hiyo ya NAM kutatua mizozo miongoni mwa masuala mengine.
Hata hivyo katika suala la mizozo, vita vya Syria vimezusha mjadala na mvutano katika mkutano huo,hasa baada ya rais wa Misri Mohammed Mursi kuwataka wanachama wa kundi hilo la NAM kuiunga mkono Syria katika juhudi za kumuondoa madarakani rais Bashar al Assad ambaye ni mshirika wa karibu sana na Iran.
Kauli ya rais wa Misri iliufanya ujumbe wa Syria kukurupuka na kutoka nje ya mkutano huo.Hata hivyo haikufahamika ikiwa ujumbe huo ulirejea tena baadae ndani ya kikao hicho. Ziara ya Mursi Tehran ni ziara ya kwanza kuwahi kufanywa na kiongozi wa Misri nchini Iran tangu mapinduzi ya nchi hiyo mwaka 1979 lakini hotuba yake inaashiria kwamba hakutakuweko maridhiano kati ya nchi hizo mbili badaa ya miongo mitatu ya uhasama.
Itakumbukwa kwamba mvutano wa Kidiplomasia kati ya Iran na Misri ulizuka mara tu baada ya mapinduzi ya Iran juu ya hatua ya Misri ya kuunga mkono kung'olewa kwa utawala wa Shah pamoja na nchi hiyo kuingia makubaliano ya amani na Israel.Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amelikosoa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa akisema ni chombo kisichokuwa na haki na kinachofuata mtazamo wa Marekani wa kuzinyanyasa baadhi ya nchi za ulimwengu.
Mwandishi:Saumu Mwasimba, rtr
Mhariri:AbdulRahman Mohammed