Hatutamtegemea Trump ili kubadili mazingira
10 Novemba 2016Washiriki wamesema hawatomkubalia rais mteule wa Marekani Donald Trump ambae ameonekana kutounga mkono makubaliano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, kuvuruga mchakato wa ulimwengu kuondokana na nishati chafu. Washiriiki hao wamesema iwapo atachukua msimamo wasiokubaliana nao basi Marekani itasalia kivyake nyuma katika hilo..Huku kukiwa na hofu kuwa rais mteule Donald Trump huenda akazingatia ahadi aliyotoa wakati wa kampeini zake ya kuiondoa Marekani katika mapatano ya Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, Australia imekuwa nchi ya hivi punde kutia saini mapatano hayo. Mapatano hayo yanalenga kukabiliana na kupanda kwa joto duniani.
Tofauti na rais Barrack Obama ambae aliyafanya mabadiliko ya tabia nchi kuwa miongoni mwa sera muhimu katika utawala wake,Trump mara kwa mara katika mitandao ya kijamii amesema kupanda kwa joto duniani ni mzaha na hakubaliani na hilo.Washiriki katika mkutano wa Morocco walikuwa na hilli la kumweleza Trump “Makubaliano ya Paris hayatamtegemea hatua ya Donald Trump, kukataa kukubali mabadiliko ya tabia nchi. Makubaliano ya Paris yatategemea uwezo wa vijana na watu wengine ulimwenguni kote kuchukua hatua” Marekani ndio ya pili duniani katika uchafuzi wa mazingira baada ya China, ikitoa asilimia 13 ya gesi chafu.
Tayari zaidi ya mataifa 100 yanayowakilisha asilimia 70 ya gesi chafu zinazozalishwa duniani yametia saini mapatano hayo ya kihistoria, yaliyoanza kutekelezwa mapema mwezi huu. Uchaguzi wa kitaifa uliofanyika nchini Australia mwezi Julai mwaka huu ndio uliochelewesha maafisa wake kutia saini mapatano hayo.Hatua hiyo itaisadia Australia kupunguza uzalishaji hewa chafu kwa kati ya asilimia 26-28 kufikia mwaka 2030. Pamoja na matumizi makubwa ya nishati inayotegemea makaa ya mawe na idadi ndogo ya watu millioni 22, Australia inachukuliwa kuwa mojawapo ya wachafuzi wakubwa wa mazingira duniani. Nayo serikali ya Ujerumani katika siku kadhaa zijazo inakamilisha utayarishaji maelezo yake yanayopaswa kuwasilishwa katika mkutano huo wa 22 wa tabia nchi unaofanyika nchini Morocco.
Waziri wa uchumi Sigmar Gabriel ambae ni kiongozi wa chama cha Social Democrat SDP chama kinachogawana madaraka na kile cha Conservative chake kansela Angela Maerkel amesema Ujerumani imedhamiria kupunguza kwa asilimia 50 utoaji wa gesi za sumu kutoka viwandani zinazoongeza kiwango cha joto duniani ifikiapo mwaka 2050. Kufikia mwaka 2030 waziri huyo amesema utoaji huo wa gesi chafu utakuwa umepunguzwa kwa asilimia 55
Mwandishi: Jane Nyingi/RTRE/AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga