Hezbollah yakana uvamizi wa Israel nchini Lebanon
1 Oktoba 2024Afif amesema hayo wakati taarifa nyingine kutoka IDF zikisema mchana huu kwamba vikosi vyake vimekuwa vikifanya uvamizi kusini mwa Lebanon kwa miezi kadhaa, na kugundua mahandaki na mipango ya uvamizi ya kundi hilo.
Mapema hii leo, jeshi la Israel, IDF lilitangaza kuanzisha operesheni ya ardhini nchini Lebanon ambayo serikali mjini Tel Aviv inasema ni muhimu ili kusambaratisha uwezo wa kundi la Hezbollah. Mbali na hayo, jeshi hilo limesema limefanya mashambulizi mapya mjini Beirut hii leo, ambayo ni ya karibuni zaidi katika msururu wa mashambulizi yanayolenga kundi la Hezbollah mjini humo.
Lakini Mkuu huyu wa ofisi ya habari ya Hezbollah Mohammad Afif ameibuka mchana huu na kusema la hasha, hakuna mwanamgambo wa kundi hilo aliyepambana moja kwa moja na mwanajeshi wa Israel na kukana madai hayo ya Israel.
Afia amesema wanamgambo wa Hezbollah wako tayari kukabiliana moja kwa moja na vikosi vya adui vitakavyojaribu kuingia Lebanon na kusababisha uharibifu.
Soma pia:Israel yaingia kijeshi Lebanon "kuisambaratisha Hezbollah"
Mbali na Afif, msemaji wa kikosi cha amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL alinukuliwa na shirika la habari la AFP akisema hakukuwa na uvamizi wowote wa ardhini kwa sasa. Naye ametoa matamshi hayo, baada ya Israel kudai kuingia Lebanon.
Mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa Ofisi ya Haki za Binaadamu ya umoja huo Liz Throssell amezungumza hii leo na kusema ofisi hiyo ina wasiwasi mkubwa juu ya msuguano baina ya Israel na Hezbollah, na zaidi sana akiangazia janga kubwa la kiutu na haki za binaadamu.
"Mvutano kati ya Israel na Hezbollah unazidi kutokota, na athari dhidi ya raia zimekwishaanza kuwa mbaya - na tunahofia uvamizi mkubwa wa ardhini wa Israel nchini Lebanon utasababisha mateso makubwa zaidi."
Mchana wa leo aidha, jeshi la Israel kupitia msemaji wake limesema limekuwa likivamia maeneo kadhaa kusini mwa Lebanon kwa miezi kadhaa sasa na kugundua mahandaki yanayotumiwa na Hezbollah pamoja na silaha zilizofichwa chini ya nyumba lakini pia wamegundua mipango ya uvamizi iliyokuwa ikifanywa na kundi hilo.
Kulingana na msemaji huyo, taarifa hizi ndio zinafichuliwa kwa mara ya kwanza.
Soma pia:Netanyahu: Hakuna eneo tusiloweza kulilenga Mashariki ya Kati
Israel yawataka wakazi wa Lebanon kuanza kuhama
Israel, katika hatua nyingine imewatahadharisha wakazi wanaoishi kwenye maeneo karibu 20 ya kusini mwa Lebanon kuondoka, hii ikiwa ni baada ya kutangaza kwamba inaanzisha uvamizi dhidi ya Hezbollah nchini humo.
Agizo hilo limechapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X na msemaji wa jeshi hilo kwa lugha ya Kiarabu, Avichay Adraee. Jamii zilizolengwa zinatakiwa kuondoka kaskazini mwa Mto Awali, kilomita 60 hivi kutoka mpaka wa Israel. Taarifa hiyo imeongeza kuwa jeshi la Israel halitaki kuwaumiza na kwa usalama wao wanalazimika kuondoka mara moja. Adraee ameandika mtu yoyote aliye karibu na mwanachama wa Hezbollah au maeneo ya Hezbollah ama hata vifaa vya kushambulia anajiweka hatarini.
Huko mjini Beirut, Waziri Mkuu wa Lebanon Najib Mikati ameutolea wito Umoja wa Mataifa kulisaidia taifa lake kupambana na kile alichotaja kama "awamu hatari kabisa katika historia." Karibu watu milioni moja nchini humo wamekwishayakimbia makazi yao kutokana na vita kati ya Israel na Lebanon, Shirika la Habari la Kitaifa limemnukuu, akisema hayo na kwa maana hiyo wanahitaji msaada.
Ofisi ya uratibu wa misaada ya kiutu ya Umoja huo, OCHA imesema asilimia 90 ya watu hao milioni moja wameondoka majumbani kwao wiki iliyopita na tayari Shirika hilo pamoja na Mikati wameanzisha mchakato wa kukusanya dola milioni 426 za msaada.
Huku hayo yakiendelea, Marekani imesema leo kwamba Iran inaandaa shambulizi la kombora la masafa marefu dhidi ya Israel, na kuionya Iran kwamba shambulizi lolote kama hilo litajibiwa "vikali". Afisa mwandamizi kwenye Ikulu ya White House ameliambia shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotambulishwa na kuongeza kuwa, Iran inajiandaa kuishambulia Israel hivi karibuni.
Soma pia:Netanyahu asema majadiliano ya kusitisha mashambulizi Lebanon yanaendelea
Na katika Ukanda wa Gaza, mashambulizi ya angani ya Israel yamewaua watu karibu 37 hii leo, vimesema vyanzo vya kitabibu wakati mapigano yakizidi kushika kasi.