1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hoffenheim yaongoza Bundesliga

28 Oktoba 2008

Ilikuaje timu ya daraja ya pili kuongoza Bundesliga ?

https://p.dw.com/p/Fj2U
Hoffenheim yatamba.Picha: picture-alliance / Pressefoto ULMER/Bjoern Hake

Bundesliga-Ligi ya Ujerumani, inarudi leo (Jumatano)uwanjani kwa mapambano 5:Viongozi wa Ligi Hoffenheim-klabu iliopanda msimu huu tu daraja ya kwanza, wana miadi na Bochum.Hertha Berlin inacheza na Hannover,Hamburg inakumbana na Stuttgart wakati mabingwa Bayern Munich, wananyatia tena kuparamia kileleni wakitumai kutamba nyumbani mwa Frankfurt.

FC Cologne, klabu nyengine kamaHoffenheim, iliopanda daraja ya kwanza kutoka ya pili msimu huu, ina miadi na Borussia Dortmund.Kinyume na Cologne ambayo miaka ya 1970 ilitawazwa mabingwa wa vikombe vyote 2 -kombe la Bundesliga na la Shirikisho la dimba la Ujerumani,Hoffenheim ni timu ya kijijini chenye wakaazi 3000 tu.

Kwamba leo ni timu ya kijijini inaongoza mojawapo ya ligi mashuhuri ulimwenguni-Bundesliga, ni maajabu kwa mashabiki wengi wa dimba. Hoffenheim imezpiku klabu kama Bayern Munich,mabingwa, Hamburg, Leverkusen na hata Bremen zinazocheza kikawaida katika vikombe vya Ulaya . Ilikuaje hata Hoffenheim kutamba namna hii ?

Kuja juu na mwishoe kuhanikiza kwa viongozi wa sasa wa Bundesliga-Hffenheim,kunatokana na mtoto wa mtaani:Dietmar Hopp,muasisi wa kampuni la software SAP na milionea.Binafsi akiichezea klabu hii ya Hoffenheim dimba. Anakumbuka:

"Naweza kukumbuka magoli maridadi kabisa niliotia na hasa zawadi niliopewa kwa kupachika mabao hayo.Nilipewa nyama tamu iliotayarishw anyumbani-wurst au hotdog."

Hopp hivi sasa ana umri wa miaka 60.Alipoizuru klabu yake ya mtaani mnamo miaka ya 1990ini,hakuweza kuamini msiba ulioifika klabu yake ya TSG-ikicheza katika ligi za wilayani.Alihisi hali hii inaweza kubadilishwa.

Kwahivyo, akaanza kazi ya kuitia jeki timu yake ya zamani.Alifanya hivyo tangu kwa fedha hata kwa kutunga mkakati jinsi ya kuinyanyua juu.Kwani, binafsi anajua vipi mafanikio yanavyostawisha mambo.Alianza kujenga kutoka msingi kwa chipukizi ,mafunzo barabara ya dimba na ujenzi wa uwanja wa mpira. Mnamo muda wa miaka 17,Hoffenheim ilipanda mara 7.

halafu akamuajiri Ralf Rangnick,mmojawapo wa makocha mashuhuri wa Bundesliga.Alihitaji kumshawishi sana kocha kama huyu kuiongoza timu yake,kwani ni kocha aliepata sifa alipoziongoza timu kali za daraja ya kwsanza za Bundesliga kama schalke ili kutoka jijini Gelsenkirchen kuja mkoani Hoffenheim.

Kocha Rangnick anasema:

"Kwa nionavyo mimi ni ile njia inayotumiwa kuja juu.Azma yetu hapa ni kutumia chipukizi wenye ustadi mkubwa wa dimba na ikiwezekana chipukizi wa kijerumani kuparamia kileleni."

Mara tu ukifanikiwa, waonao wivu hawakawii kuchomoza:Tunapocheza ugenini ,asema kocha Rangnick,hatukosi kuambiwa ni fedha za Hopp ndio Hoffenheim imemudu mafanikio haya.Mara kwa mara , hufananishwa na FC Chelsea ya Uingereza.Hopp hakubaliano nao:

"Kwanza mkwiji wa Abramovic ni mkubwa zaidi kuliko wangu.Pili, tunatofautiana kifalsafa.

Mimi sijanunua klabu ,bali nimetia raslimali yangu kwa chipukizi wa klabu hii,pia nimeekeza katika klabu ya kwanza ambayo yapaswa kuwa mfano kwa vijana.Abramovic shabaha yake sio hiyo.Abramovic amenunua klabu tayari mashuhuri na inayocheza ligi tofauti.Isitoshe, hiyo sio staili yangu hata ningekua nina fedha kama hizo."

Hopp ametjga mkakati maalumu ambao kila nafasi inashikwa na mabingwa wa fani yake: Hans-Dieter Hermann,mtaalamu wa saikolojia wa timu ya Taifa ya Ujerumani ni mmojawao.Halafu kuna Bernhard Peters, kocha wa mabingwa wa dunia-timu ya hoki ya Ujerumani ndie anaeongoza shughuli za vijana katika ti mu ya Hoffenheim.

Kwamba Hoffenheim, itakuja juu haraka namna hivyo hadi leo inaongoza Bundesliga,hakuna hata wenye tamaa walidhania .Kocha ralf rangnick sasa amezomngwa na kazi nyingi kuokoa timu yake isiteremke chini.Anasema :

"Timu yetu isiangalie wapi ilipo katika ngazi ya Ligi bali ijishughulishe n a jinsi ya kushinda mechi ijayo."

Hakuna kwahivyo haja ya kumuuliza kocha Rangnick nini shabaha yake msimu huu:Shabaha inakuja wenyewe.Mbali na mafanikio ya kispoti kuna kitu kingine kiliopo moyoni mwa mkubwa wa Bw.Rangnick -Dietmar hopp:

"Nina shabaha moja" asema Hopp-TSG Hoffenheim igeuke kampuni ambalo linajiendesha wenyewe kwa uwezo wake.Raslimali gani itahitajika kwa timu hii hadi kufikia shabaha hiyo, hajui kwa sasa...

Jambo moja liko wazi, msimu ujao Hoffenheim haitaendelea kucheza katika Uwanja wa Mannheim.Kwani hadi wakati huo, Hoffenheim itatamba katika uwanja wake utakaochukua mashabiki 30.000 .