1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hoffenheim yatoka sare na Dortmund

17 Desemba 2016

Baada ya mchezo kama huu, Borussia Dortmund inapaswa kuweka kipengele kipya katika mkataba wa Ousmane Dembele ili kuwa vigumu kwa yeyote anayetaka kumsajili

https://p.dw.com/p/2URgv
1. Bundesliga 15. Spieltag - TSG 1899 Hoffenheim vs.  Borussia Dortmund | Tor Hoffenheim
Hoffenheim walisonga hadi nafasi ya tatuPicha: picture-alliance/dpa/U. Anspach

Hoffenheim 2-2 Borussia Dortmund
(Uth 3, Wagner 20 - Götze 11, Aubameyang 48)

Baada ya mchezo kama huu, Borussia Dortmund inapaswa kuutathmini upya kwa kuweka masharti mapya katika mkataba wa Ousmane Dembele ili kuwa vigumu kwa yeyote anayetaka kumsajili. Chipukizi huyo Mfaransa, ambaye ana umri wa miaka 19 pekee, alionyesha mchezo wake mzuri zaidi tangu alipojiunga na klabu hiyo ya Bundesliga akitokea Rennes mwaka huu, na ushahidi tosha kuwa ni mmoja wa vijana wenye kipaji wanaoimarika.

Alimpa pasi Mario Götze ambaye alifunga bao lake la kwanza la Bundesliga tangu aliporejea Dortmund, na nyingine Pierre-Emerick Aubameyang iliyomwezesha mshambuliaji huyo kutia kimyani bao la pili.

Lakini sio tu pasi hizo mbili zilizofanya aangaziwe sana katika uwanja wa Rhein-Neckar. Kasi yake na motisha ndivyo vitu muhimu katika mfumo wa kocha Thomas Tuchel wa kufanya mashambulizi na kulikuwa na nyakati ambazo Hoffenheim walishindwa kumkaba.

Ilisikitisha sana kuona Dembele akiondolewa uwanjani kwenye machela katika kipindi cha pili baada ya kupata jeraha ambalo Dortmund itatumai kuwa sio baya sana.

Dembele alihitaji kujaza pengo, wakati Marco Reus alitimuliwa uwanjani katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza kwa kuonyeshwa kadi mbili za njano katika mchezo wake huo wa nne wa Bundesliga.

Lakini Hoffenheim ilianza mchezo huo kwa kasi na kuwapa mashabiki sababu ya kupaza sauti uwanjani ndani ya dakika tatu wakati kipa wa Dortmund Roman Weidenfeller alijikuta nje kabisa ya lango lake na kumwezesha Mark Uth kufunga bao katika mlango wazi.

1. Bundesliga 15. Spieltag - TSG 1899 Hoffenheim vs.  Borussia Dortmund | Reus Gelbe Karte
Reus alionyeshwa kadi mbili za njanoPicha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Uongozi wa Hoffenheim ulidumu kwa dakika nane pekee wakati Dembele alimpa pasi Götze ambaye alitikisa wavu ndani ya eneo hatari.

Dortmund walidhibiti mambo lakini hawakufunga bao na kuwaruhusu Hoffenheim kurejea tena kifua mbele kupitia bao la Sandro Wagner. Lakini Dortmund ikiongozwa na Dembele, ilianza kipindi cha pili kwa kasi na kusawazisha kupitia bao la Aubameyang

RB Leipzig wanaweza kukamata tena nafasi ya kwanza wakati watawaalika Jumamosi nambari nne kwenye ligi hiyo Hertha Berlin. Bayern Munich ambao wanaongoza pointi sawa na Leipzig japo kwa faida ya mabao, watashuka dimbani kesho Jumapili dhidi ya Darmstadt. Nchini  England, kocha wa Manchester City Pep Guardiola amethibitisha kuwa kiungo Ilkay Gündogan anahitaji upasuaji wa goti maana kuwa Mjerumani huyo anakabiliwa na kipindi kirefu mkekani.

Mechi za Jumamosi

Mainz  v Hamburg SV

Augsburg  v Borussia Moenchengladbach

RB Leipzig v Hertha Berlin 

Schalke 04 v Freiburg

Werder Bremen v Cologne   

VfL Wolfsburg v Eintracht Frankfurt

Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Sekione Kitojo