1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hollande aapa kuendeleza mageuzi ya ajira

27 Mei 2016

Rais wa Ufaransa Franocis Hollande ameapa kuendelea na mageuzi yanayopingwa ya sekta ya kazi nchini humo. Vyama vya wafanyakazi vimewataka wafanyakazi waendeleze migomo dhidi ya sheria hizo tata

https://p.dw.com/p/1Iv80
Frankreich Arbeitsmarktreform Protest
Picha: Getty Images/AFP/F. Lo Presti

Akizungumza pembezoni mwa mkutano wa viongozi wa kundi la mataifa saba yenye ustawi wa kiviwanda duniani – G7 nchini Japan, Rais Hollande ameahidi kuendelea na mipango yake ya mageuzi hayo ya sekta ya ajira, licha ya migomo ya wafanyakazi ambayo imevuruga shughuli za kawaida nchini humo. Amesema serikali yake itahakikisha „uhuru wa kutembea kwa raia wake walioathirika na migomo ya wafanyakazi wa safari za reli nchini humo na kufungwa vituo vya mafuta.

Ikiwa imesalia wiki mbili tu kabla ya Ufaransa kuandaa dimba la Kombe la Mataifa ya Ulaya Euro 2016, nchi hiyo imekumbwa na migomo iliyodumu zaidi ya wiki moja ambayo imevuruga usafiri na kusababisha uhaba wa mafuta.

Hali ya vuta nikuvute kati ya vyama vya wafanyakazi na serikali ya Rais Francois Hollande iliyopoteza kabisa umaarufu imeonyesha dalili chache mno za kufikia kikomo, wakati wawakilishi wa vyama wanawataka wafanyakazi kujitokeza kwa wingi na kuunga mkono migomo hiyo.

Wanasema namna ambavyo serikali inaishughulikia migomo hiyo na „ukaidi“ wake kwa kukataa kuondoa sheria hiyo inayopingwa kunachangia katika kuimarisha ari ya wanaopinga sheria hiyo.

Frankreich Geschlossene Tankstelle in Savenay
Migomo imesababisha uhaba mkubwa wa mafutaPicha: Reuters/S. Mahe

Waziri Mkuu Manuel Valls alisema serikali haitaibatilisha sheria hiyo lakini itafanya marekebisho ya hapa na pale lakini sio kuhusu vipengele muhimu.

Alhamisi, polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi kulitawanya kundi dogo la vijana waliofunika nyuso zao ambao waliyaharibu maduka na magari yaliyoeegeshwa katikati ya Paris. Polisi imesema maandamano ya jana kote Ufaransa yalihudhuriwa na watu 153,000 ijapokuwa vyama vya wafanyakazi vimeiweka idadi kuwa watu 300,000.

Vyama vya wafanyakazi vina hasira kuhusu sheria iliyopitishwa kwa nguvu bungeni inayolenga kuzifanyia mageuzi sheria ngumu za kazi nchini Ufaransa kwa kuziwezesha kampuni kuwaajiri na kuwafuta kazi wafanyakazi kwa urahisi. Mashirika mengi ya kimataifa, likiwemo Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF, yanasema sheria hizo za kazi ni muhimu katika kuweka nafasi za kazi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo