Hollande aitaka Israel iache ujenzi wa walowezi
18 Novemba 2013Katika mtindo wa kuuma huku akivungia, Rais Hollande aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kati yake na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina kwamba nchi yake inataka Israel isitishe kabisa ujenzi huo wa makaazi ya walowezi na akarejea msimamo wa nchi yake kwamba ulinzi pekee na amani ya Israel ni kuwepo kwa dola huru ya Palestina.
"Kwa maslahi ya amani na kufikia makubaliano, Ufaransa inataka pasitishwe kabisa ujenzi wa makaazi hayo kwani inaliweka hatarini suluhisho la dola mbili huru." Alisema Hollande.
Lakini, kwa upande mwengine, Hollande amewakumbusha Wapalestina kwamba wanapaswa wenyewe kutafuta suluhisho la suala la wakimbizi, ambalo amesema bila ya hilo hakutakuwa na makubaliano kati ya pande hizo mbili.
Pamoja na utanuzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi, suala la kurudi kwa mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina kwenye ardhi yao iliyochukuliwa kwa nguvu na Israel, ni mambo yanayoyakwamisha kila mara mazungumzo ya kusaka suluhu. Hollande amesema "hakutakuwa na dola ya Kipalestina kama usalama wa Israel hautahakikishwa."
Israel yaendelea na mipango ya ujenzi
Tayari Israel imeshatangaza mipango ya kujenga maelfu ya makaazi mapya ya walowezi tangu kuanza kwa mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani hapo Julai, baada ya miaka mitatu ya kuvunjika kwake.
Wajumbe wa timu ya Wapalestina kwenye mazungumzo hayo wameomba kujiuzulu wakipinga hatua hiyo ya ujenzi, lakini Rais Abbas amethibitisha kwenye mkutano huo na waandishi wa habari kwamba mazungumzo hayo yataendelea kwa kipindi cha miezi tisa kamili kama walivyokubaliana na mpatanishi, Marekani.
Jana (17 Nov.), Hollande alikuwa na mazungumzo na viongozi wa Israel mjini Jerusalem, na asubuhi ya leo akakutana na Rais Abbas katika makao makuu ya utawala wa ndani ya Palestina, Ukanda wa Magharibi.
Wapalestina wanapigania kuanzisha dola yao kwenye Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, ambao kwa sasa uko chini ya udhibiti wa kundi la Hamas, na Jerusalem ya Mashariki ukiwa mji wao mkuu. Wanahofia kwamba ujenzi wa makaazi ya walowezi ukawa kikwazo cha kuwa na taifa lao wenyewe.
Zaidi ya Waisraili 500,000 wanaishi kwenye Ukingo wa Magharibi na Jerusalem ya Mashariki sambamba na Wapalestina milioni 2.5.
Waisraeli wanadai wana haki ya miji hiyo kwa mujibu wa Biblia, lakini mataifa mengi duniani wanayachukulia makaazi yaliyojengwa na Israel katika ardhi iliyoziteka kwenye vita va mwaka 1967 kuwa ni haramu.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf