1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Homa ya uchaguzi wa bunge la Ulaya yapanda

Oumilkheir Hamidou
7 Novemba 2018

Jinsi ya kuwahamasisha wapiga kura kuelekea uchaguzi wa Ulaya mwaka 2019, mjadala kuhusu mkataba wa umoja wa mataifa kuhusu wakimbizi na mvutano wa bajeti katai ya Italia na Umoja wa Ulaya magazetni.

https://p.dw.com/p/37o22
Frankreich EU-Menschenrechtspreis an Oleg Senzow
Picha: picture-alliance/AP Photo/J.-F. Badias

Tunaanza na jinsi wanasiasa wa vyama tofauti wanavyojiandaa kuelekea uchaguzi wa bunge la Ulaya utakaoitishwa mwaka 2019. Gazeti la "Aachener Nachrichten" linaandika: "Miezi inayokuja itadhihirisha jamii inafuata mkondo gani na kama inaweza kukubaliana na changamoto zilizoko. Kama inaweza kusaka ufumbuzi, kuimarisha mshikamano , kuwapa atu moyo na kuepusha balaa la kuendewa kinyume misingi ya Ulaya ambayo ni pamoja na mshikamano, uhuru na dola linalofuata sheria. Uchaguzi wa bunge la Ulaya mwaka 2019 unaweza kufungua njia muhimu kuelekea shabaha hiyo.

Muhimu zaidi itakuwa idadi ya watakaoteremka vituoni. Mwaka 2014 asili mia 47.9 tu ndio walioteremka vituoni nchini Ujerumani na kwa mtazamo jumla barani Ulaya idadi yao haikupundukia asili mia 42.54. Idadi ndogo ya wapiga kura itawanufaisha wale wanaoupinga umoja wa Ulaya .Tunapendelea kuwa na Umoja wa Ulaya wa aina gani, suala hilo, itakuwa vizuri tukilijibu sisi wenyewe badala ya kuwaachia peke yao wanasiasa."

Mkataba wa Umoja wa mataifa kuhusu wakimbizi watiwa ila

Sera kuelekea wakimbizi na wahamiaji ndio mada kuu inayotumiwa na makundi ya siasa kali kuanzia Ujerumani hadi katika nchi nyengine za Umoja wa ulaya. Mjadala umepamba moto na kuutia ila  mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika: "Ingawa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesaidia kufikiwa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi, imeshindwa lakini kuzuwia suala hilo lisitumiwe vibaya .Ingawa makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia kwa miezi kadhaa sasa yanaeneza chuki dhidi ya wahamiaji na wakimbizi, serikali kuu haijajitetea badala yake imewaachia uwanja AfD na wengine kama hao. Pengine kwa uzembe au kwa hofu ya kuzuka mjadala. Sasa mambo yamewageukia. Wafuasi wa siasa kali ya mrengo wa kulia wanaitumia mada hiyo kujipatia umashuhuri."

Italia yaregeza kamba

Mada yetu ya mwisho magazetini inatupeleka Brussels ambako mvutano wa bajeti kati ya umoja wa ulaya na Italia unaashiria huenda ukapatiwa ufumbuzi.Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linaandika: "Serikali inayofuata siasa kali za kizalendo ya Italia mjini Roma imeonyesha dalili ya kutaka kuzungumza sasa . Imeamua kuitoa Italia katika hali ya upweke na kukiri Umoja wa ulaya usaidie katika kubuni bajeti ya maana itakayoitoa nchi hiyo katika hali ya mzozo. Sio tu uchumi wa Italia utafaidika, hali jumla itaimarika kuelekea uchaguzi wa bunge la ulaya may mwaka 2019."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi ssessanga