Horst Seehofer, mkuu wa CSU kuachia madaraka
16 Novemba 2018Katika taarifa ya maandishi iliyochapishwa mjini Munich, mwanasiasa huyo wa siku nyingi mwenye umri wa miaka 69 amesema kuwa mkutano wa dharura wa kumchagua mwenyekiti mpya wa chama hicho utaitishwa Januari 19 mwakani na kuongeza kuwa mwaka 2019 utakuwa wa mageuzi kwa chama cha CSU.
Ingawa taarifa hiyo ya leo haikutoa maelezo yoyote juu ya hatma ya wadhifa wake wa waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu mjini Berlin, duru za shirika la habari la DPA zimesema, Seehofer aliwaarifu viongozi wa ngazi ya juu wa chama cha CSU jumapili iliyopita kuwa analenga vilevile kuwachia nafasi hiyo.
Uamuzi wa Seehofer unakuja wiki kadhaa baada ya Kansela Angela Merkel kutangaza kuwa atajiuzulu wadhifa wake wa kiongozi wa chama cha kihafidhina cha
Christian Democrats (CDU), na muhula wake akiwa Kansela unaomalizika mwaka 2021 utakuwa wa mwisho.
Seehofer alikabiliwa na shinikizo kubwa
Uungwaji mkono CSU, ambacho ni chama ndugu cha CDU cha Kansela Merkel kinachoendesha pekee siasa zake katika jimbo la kusini mashariki la Bavaria umeporomoka kwa asilimia kumi kwenye uchaguzi wa bunge la jimbo la Bavaria mwezi uliopita na kupoteza wingi wa wabunge kwenye chombo hicho.
Majibizano ya hadharani kati ya Seehofer na Merkel juu ya suala la uhamiaji na ulinzi wa mipaka mapema mwaka huu umetajwa kuwa chanzo cha kuporomoka kwa umashuhuri na matokeo mabaya ya uchaguzi kwa vyama vinavyoongoza serikali ya shirikisho vya CDU/CSU na mshirika wao SPD.
Kujiuzulu kwa Seehofer kama kiongozi wa CSU ni ishara kuwa amekubali shinikizo kubwa alilopata kutoka kwa chama chake baada ya kupungua kwa idadi ya kura kwenye uchaguzi wa bunge wa mwezi Septemba mwaka 2017 na uchaguzi wa majimbo wa katikati ya mwezi Octoba mwaka huu.
Hakuna hadi sasa mwanasiasa aliyetangaza kumrithi Seehofer katika wadhifa wa uenyekiti lakini Markus Soeder anapewa nafasi ya mbele walau kwa hivi sasa.
Merkel anakwenda Chemnitz
Wakati hayo yanajiri, kansela wa Ujerumani bibi Angela Merkel anauzuru mji wa mashariki ya Ujerumani wa Chemnitz leo miezi mitatu tangu shambulio la kisu lilipozusha siku kadhaa za maandamano makubwa kutoka makundi yanayopinga na yanayounga mkono wahamiaji.
Matukio ya Chemnitz ni moja ya mzozo wa karibuni kabisa uliosababisha kuunguka uungwaji mkono wa vyama vinavyounda serikali kuu ya ujerumani kwenye uchaguzi wa majimbo na uamuzi wa baadae wa bibi Merkel kutangaza kujiuzulu uenyekiti wa chama cha CDU.
Mwandishi: Rashid Chilumba/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman