HRW haikuridhishwa hukumu mauaji maafisa wa Umoja wa Mataifa
7 Februari 2022Ripoti iliyotolewa Jumatatu (Februari 7) na shirika hilo imesema kwamba hata baada ya msaada mkubwa wa Umoja wa Mataifa, mahakama nchini Kongo ilipuuzia ushahidi uliooteza vidole kwa maafisa wa ngazi za juu wa serikali.
"Kwenye kipindi chote cha miaka minne ya kesi hii, upande wa mashitaka kamwe haukuchunguza waliopanga na kuamuru mauaji ya wataalamu hawa wa Umoja wa Mataifa," alisema mtafiti wa ngazi za juu wa Human Rights Watch nchini Kongo, Thomas Fessy, ambaye ameongeza kwamba "Umoja wa Mataifa, Marekani na Sweden zinapaswa kutambua kushindwa huko kwa Kongo na kuchunguza kikamilifu uhalifu huu."
Tarehe 29 Januari 2022, mahakama ya kijeshi ya Kananga iliwahukumu kifo watuhumiwa 49, wengi wao wakiwa hawapo mahakamani hapo, kwa ugaidi, mauaji, na uhalifu wa kivita.
Afisa wa kijeshi mwenye cheo cha kanali, Jean de Dieu Mambweni, alihukumiwa kifungo cha miaka kumi kwa kutokufuata amri, huku afisa wa uhamiaji, Thomas Nkashama, akiwa miongoni mwa waliohukumiwa kifo na washukiwa wawili waliondolewa hatia.
Mauaji ya Catalan na Sharp
Mnamo tarehe 12 Machi 2017, watu wasiojulikana waliwauwa Zaida Catalan, raia wa Sweden, na Michael Sharp, raia wa Marekani, wakati walipokuwa wakichunguza uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu na pia wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa katika mkoa wa Kasai Central.
Catalan na Sharp walikuwa wakilifanyia kazi jopo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo walinda amani wa Umoja huo waliipata miili yao wiki moja baadaye katika kijiji cha Bukonde.
Mkalimani wao wa Kikongo, Betu Tshintela, pamoja na madereva watatu wa bodaboda waliokuwa wakiwasindikiza bado hawajulikani walipo hadi leo.
Kesi hiyo ilianza mwezi Juni 2017 katika mahakama ya kijeshi ya Kananga, mji mkuu wa jimbo hilo, na timu maalum ya Umoja wa Mataifa imekuwa ikitowa msaada wote unaohitajika.
Ghasia za Kasai
Ghasia baina ya makundi ya kikabila zilizuka mkoani Kasai mwaka 2016, ambapo mzozo huo ulihusishwa na siasa za kitaifa, ambapo jeshi la Kongo liliwasadia wale waliotazamwa kama wanamuunga mkono rais wa wakati huo, Joseph Kabila na muungano wake wa kisiasa, huku baadhi ya wanamgambo wakiiunga mkono walio karibu na upinzani.
Mamia waliuawa kwenye machafuko hayo na zaidi ya watu laki mbili walilazimika kuyakimbia makaazi yao.
Licha ya awali serikali ya Kabila kuwahusisha wanamgambo wa Kamulina Nsapu kwa mauaji hayo ya Catalan na Sharp, lakini ushahidi ulioibuliwa kupitia mashirika mbalimbali ya habari uliwahusisha maafisa wa ngazi za juu serikali na mauaji hayo.