1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Kuna ushahidi wa mateso Jamhuri ya Afrika ya Kati

Josephat Charo
3 Mei 2022

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema vikosi vya Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambao mashahidi waliwatambua kama Warusi, wanaonekana waliwaua, kuwatesa na kuwapiga raia tangu mwaka 2019.

https://p.dw.com/p/4AmIz
Human Rights Watch | Logo
Picha: John MacDougall/AFP/Getty Images

Wataalamu wa serikali kadhaa za nchi za magharibi na Umoja wa Mataifa pamoja na wajumbe maalumu wamegundua ushahidi kwamba vikosi vyenye mafungamano na Urusi vinavyoendesha shughuli zao katika Jamhuri ya Afrika ya Kati vinajumuisha idadi kubwa ya wanachama wa kampuni ya Wagner Group, kampuni ya kibinafsi ya masuala ya ulinzi wa kijeshi yenye mafungamano na serikali ya Urusi. Mnamo Aprili 15 Umoja wa Mataifa ulitangaza ungechunguza mazingira ambapo watu 10 waliuliwa eneo la kaskazini mashariki, huku ripoti za awali zikidai maafisa wa vikosi va Urusi huenda walihusika.

Ida Sawyer, mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch anayehusika na masuala ya mizozo amesema kuna ushahidi kwamba vikosi vilivyotambuliwa kuwa vya Warusi vimefanya vitendo vya mateso na unyanyasaji wa raia bila kuwa na hofu ya kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Sawyer aidha amesema kushindwa kabisa kwa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na washirika wake kulaani kwa nguvu vitendo hivi na kutambua na kuwashitaki wahusika, huenda kwa kiwango kikubwa kukachochea uhalifu zaidi barani Afrika na kwingineko.

HRW yawahoji walioshuhudia

Kati ya Februari 2019 na Novemba 2021, Human Rights Watch iliwahoji watu 21 ana kwa ana na wengine 19 kwa njia ya simu, wakiwamo wahanga 10 na mashuhuda 15, kuhusu mateso na udhalilishaji waliosema ulifanywa na wanaume wenye ngozi nyeupe wanaozungumza lugha ya Kirusi, ambayo wanasema waliitambua. Watu walioshuhudia wanasema wanaume hao walikuwa wamebeba silaha nzito zinazotumiwa na jeshi na walivalia nguo za khaki, vitambaa kufunika nyuso zao, viatu vya kijeshi, glavu na miwani ya kujikinga na jua.

Afrika Menschen fliehen vor Gewalt in Zentralafrika
Mwanamume akiyakimbia machafuko katikati ya Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: AP Photo/picture alliance

Mwezi Agosti mwaka 2018, Jamhuri ya Afrika ya Kati na maafisa wa Urusi walitia saini mkataba ambapo maafisa wa zamani wa kijeshi kutoka Urusi, ambao huitwa wataalamu, wangetoa mafunzo kwa vikosi vya nchi hiyo ya Afrika. Vikosi vyenye mafungano na Urusi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati hawavai sare maalumu na mavazi rasmi wala viashiria vinavyowatofautisha.

Watu 12 walizungumzia tukio la asubuhi ya Julai 21 mwaka uliopita ambapo vikosi vya Urusi viliwaua watu wapatao 12 karibu na mji wa Bossangoa. Shirika la Human Rights Watch lilipata majina ya waliouwawa kutoka kwa Umoja wa Mataifa na wengine waliowafahamu wahanga. Shirika hilo pia limeorodhesha visa vya watu kuzuiliwa na kuteswa na vikosi vyenye mafungamano na Urusi huko Bambari mnamo mwaka 2019.

Mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch anayehusika na masuala ya mizozo, Ida Sawyer, ametoa wito madai ya msingi kuhusu mateso, yakiwamo visa vinavyoweza kuorodheshwa kama uhalifu wa kivita vilivyofanywa na vikosi vya Urusi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati vichunguzwe na wahusika wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria. Ameitaka Urusi ishirikiane kikamilifu katika uchunguzi wa aina hiyo.

(hrw)