HRW yasema kundi la RSF lahusika katika ubakaji Darfur
17 Agosti 2023Tangu kuanza kwa mzozo wa kivita nchini Sudan kati ya wanajeshi wa Sudan na kikosi cha wanamgambo wa RSF mnamo Aprili 15 Aprili, kikosi hicho na wapiganaji wengine washirika wa Kiarabu wameendesha mashambulizi ya mara kwa mara katika miji na vijiji kwenye jimbo la Darfur Magharibi. Mashambulizi haya yamelenga zaidi maeneo yanayokaliwa na mojawapo ya jamii za watu wasiokuwa wa kabila la Massalit.
Soma pia: Vita Sudan havionyeshi dalili ya kuisha miezi minne baadae
Kikosi cha wanamgambo cha RSF na washirika wake chadaiwa kuhusika katika maasi Darfur
Belkis Wille, mkurugenzi mshirika anayeshughulikia migogoro katika shirika la Human Rights Watch, amesema kuwa kikosi cha RSF na washirika wake, kinaonekana kuhusika na idadi ya visa vya ubakaji na uhalifu mwingine wa kivita wakati wa mashambulizi dhidi ya El Geneina. Wille amesema kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kuwaonesha wale waliohusika katika unyanyasaji huo kwamba ulimwengu unatazama kwa kuchukuwa hatua za haraka kukomesha maasi hayo.
Human Rights Watch yawahoji waathiriwa
Mwishoni mwa nwezi Julai, Human Rights Watch iliwahoji wanawake tisa nchini Chad na msichana mwenye umri wa miaka 15 kutoka El Geneina ambao ni waathiriwa wa ubakaji huo na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia.
Soma pia :Jenerali wa juu wa Sudan amshutumu mpinzani wake kwa uhalifu na kuwadanganya raia
Wanne, akiwemo msichana huyo, walibakwa na wanaume wengi. Kulingana na matukio binafsi ya waathiriwa hao na visa walivyoshuhudia, pamoja na maelezo yaliyotolewa na watoa huduma ikiwa ni pamoja na maeneo ambapo matukio hayo yalitokea, Human Rights Watch iliwaorodhesha waathiriwa 78, au walionusurika ubakaji kati ya Aprili 24 na Juni 26.
Makundi ya wavamizi yavalia sare ya RSF
Manusura waliozungumza na shirika hilo la Human Rights Watch, wamesema kuwa kati ya mshambuliaji mmoja hadi sita walitekeleza unyanyasaji wa kijinsia. Vikundi vingi vya wavamizi vilijumuisha wanaume waliovalia sare kamili au zisizo kamili za RSF na baadhi, walivalia nguo za raia. Wakati mwingi, waliwasili kwa kutumia magari yaliokuwa na alama ya RSF. Mwanamke mmoja alimtambua mvamizi wake kuwa mkazi wa Kiarabu wa El Geneina
Soma pia:Mapigano ya Sudan yanazidi kulididimiza taifa hilo
Waliohusika na ubakaji pia wafanya unaynyasaji nwingine
Katika karibu matukio yote yaliyoripotiwa na Human Rights Watch, wale waliohusika na ubakaji pia walifanya unyanyasaji mwingine mkubwa ikiwa ni pamoja na kupiga, mauaji, uporaji, au kuchoma moto nyumba, biashara au majengo ya serikali. Watu wote walionusurika wanasema kwamba washambuliaji hao walitaja makabila yao na kutumia matusi ya kikabila kuhusu Wamassalit au wasio Waarabu.
Sheria ya kimataifa ya kibinadamu, inayoitwa sheria ya vita, inakataza wahusika kwenye mzozo wa kivita kuwadhuru raia kwa makusudi. Kifungu cha 3 katika Makubaliano ya Geneva ya 1949 na sheria ya kimataifa ya kitamaduni kuhusu haki za binadamu ambazo zote zinatumika kwa pande zote zinazopigana nchini Sudan, zinakataza ubakaji na aina zingine za unyanyasaji wa kijinsia.