1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: SCC mwanzo wa haki Afrika ya Kati

12 Aprili 2022

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema kuanza kesi ya kwanza kwenye Mahakama Maalum ya Uhalifu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (SCC) ni mwanzo wa kusaka haki ya wahanga wa uhalifu wa kivita nchini humo.

https://p.dw.com/p/49pKf
DW Premium Thumbnail | Zentralafrikanische Republik | Kind in Vertriebencamp
Picha: © Zigoto Tchaya/DW

Kesi itakayosomwa Jumanne (Aprili 19) inahusisha makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu yaliyotendeka mnamo mwezi Mei 2019 katika miji ya Koundjili na Lemouna.

Katika matukio ambayo shirika la Human Rights Watch iliyarikodi, wapiganaji watatu wa kundi la waasi lililoitwa "3R" wanapandishwa mahakamani kujibu mashitaka dhidi yao. Wapiganaji hao ni Issa Sallet Adoum, Ousman Yaouba na Tahir Mahamat.

Wakili wa ngazi za juu wa sheria za kimataifa katika Human Rights Watch, Esti Tambay, amesema kesi hii ya kwanza na hatua muhimu kwa wahanga nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao wamekuwa wapigania haki kutendeka dhidi ya uhalifu wa kinyama uliontendeka wakati wa migogoro iliyofululiza nchini humo.

 "Mahakama hii ya aina yake, ambayo inachanganya uzoefu wa kimataifa na wa ndani kuwawajibisha waliohusika na uhalifu huu mkubwa, inaweza kuwa kigezo muhimu cha haki cha kufuatwa na mataifa mengine." Aliongeza wakili huyo.

Jukumu la SCC

Mahakama hiyo Maalum ya Uhalifu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (SCC) ilianza kazi rasmi mwaka 2018 ili kusaidia kuzuwia kiwango kikubwa cha hali ya wakosaji kutochukuliwa hatua kwa makosa makubwa ya uhalifu nchini humo.

Zentralafrikanische Republik Symbolbild Kinder Mine
Hali ya umasikini wa kutupwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati inachangia pakubwa mapigano na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.Picha: Issouf Sanogo/AFP

Mahakama hiyo ina majaji na waendesha mashitaka wa ndani na wa kimataifa na gharama zake hulipwa na msaada wa kimataifa.

Ina mamlaka ya kutoa hukumu kwa makosa ya uhalifu mkubwa uliotendeka wakati wa mapigano yaliyoanza tangu mwaka 2003.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, mahakama ya SCC inafanya uchunguzi wake kwa misingi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ambayo kwa sasa ina watuhumiwa wannewanaoshitakiwa kwa makosa yaliyofanyika nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Human Rights Watch imesema kwenye taarifa yake ya maswali na majibu kwa waandishi wa habari iliyotolewa Jumanne (Aprili 12), kwamba ambapo ICC inaweza kuwa na jukumu muhimu kwa kusikiliza kesi zinazohusu uongozi wa juu wa makundi yaliyohusika na uhalifu huo, SCC inajikita kwenye kuendesha kesi ambazo ushahidi wake ulikusanywa zaidi katika mji mkuu, Bangui.

Tambay alisema SCC ni mfano halisi wa mahakama ambazo zinahitajika kwenye mataifa yote ambayo yamepitia hali kama ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kwamba serikali zina wajibu wa kuzifadhili mahakama za aina hiyo, kufanya uchunguzi na kuwakamata watuhumiwa.