1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Serikali za Afrika ziwekeze kwenye elimu ya watoto

16 Juni 2021

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch limezitaka serikali barani Afrika zimetakiwa kuharakisha juhudi na kuwekeza fedha za kutosha kuhakikisha kuwa watoto wote wanaweza kufaidi fursa ya kupata elimu.

https://p.dw.com/p/3v1UK
Kamerun Kumba Schüler bei PC-Unterricht
Picha: imagebroker/imago images

Licha ya hatua muhimu kuchukuliwa katika miongo ya hivi karibuni kuhakikisha kuwa Mkataba wa Afrika juu ya Haki na Ustawi wa Watoto unaridhiwa kote barani humo, shirika la Human Rights Watch linasema watoto wengi bado wananyimwa haki yao ya kimsingi ya kupata elimu. 

Idadi hiyo inajumuisha maelfu ya wasichana wanaokabiliwa na vikwazo kadhaa, ukiwemo ujauzito, malezi, ama ndoa za utotoni. 

Kwa mujibu wa shirika hilo, watoto kwenye mataifa 18 ya Afrika wanaathirika na mashambulizi ya watu wenye silaha na skuli zao kutumiwa kwa shughuli za kijeshi.

"Watoto kote Afrika wanakabiliwa na unyanyasaji na vikwazo vilivyoshikana pamoja kila siku dhidi ya haki yao ya elimu. Mamilioni ya watoto wametengwa ama wamewacha nyuma kwenye masomo wakati wa janga la corona, na athari zake za kiuchumi zimewalazimisha wengi kufanya kazi za hatari, jambo ambalo pia huwalazimisha kuacha masomo." Alisema mkurugenzi wa utetezi wa shirika hilo kanda ya Afrika, Carine Kaneza Nantulya.

Dhima ya Muungano wa Afrika

Maudhui ya mwaka huu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa Muungano wa Afrika yanajikita kwenye kuharakisha utekelezaji wa Ajenda 2040, ambayo inatilia mkazo utayarifu wa Muungano huo katika kuhakikisha maendelo ya vijana na watoto. 

Kinderehe in Afrika | Elfenbeinküste
Human Rights Watch inaziomba serikali za Afrika kutekeleza kikamilifu Mkataba wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa Afrika.Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Kuhakikisha haki ya elimu bure, lenye sifa na inayojumuisha na kupunguza ukosefu wa usawa katika kupatikana kwa elimu ni kitu cha muhimu sana kwenye kuipeleka mbele ajenda hiyo.

Hata kabla ya janga la COVID-19, mataifa ya Afrika yaliyo kusini mwa Jangwa la Sahara yalishakuwa na idadi kubwa zaidi ya watoto wanaoacha masomo na waliotengwa. 

Watoto milioni 32 wa umri wa kwenda skuli za msingi na milioni 28 wa umri wa kwenda skuli za sekondari, walikuwa hawapo madarasani. 

Kufungwa kwa masomo kutokana na janga hilo na kukosekana fursa ya kusoma mtandaoni, kumeongezea tu ukosefu wa usawa wa kielimu ambao tangu hapo ulishakuwepo.

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, mamilioni ya watoto barani Afrika wanakabiliwa sasa na vikwazo vya kifedha, kijamii na hata ubaguzi na wako hatarini kujikuta wametengwa kupata fursa ya elimu nzuri, hasa wasichana, watoto wenye ulemavu, watoto kutokea familia za kipato cha chini na wale wanaoishi kwenye maeneo yenye mapigano.