1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Uganda inaendeleza ukiukwaji wa haki

22 Machi 2022

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeilaumu serikali ya Uganda kwa kuendeleza mateso yanayohusiana na raia kukamatwa, kutoweka na kuzuiliwa bila kufikishwa mahakamani.

https://p.dw.com/p/48pPZ
Uganda Kriminalität l Stella Nyanzi l Frauenprotest in Kampala
Picha: Frederic Noy

Serikali ya Uganda imeshindwa kuwawajibisha maafisa wa usalama ambao wanahusika na kuwakamata na kuwatesa, wakosoaji wa serikali, wafuasi wa upinzani walioandamana kwa amani na watu wengine. Hayo ni kulingana na ripoti ambayo imetolewa leo na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch.

Ripoti hiyo yenye kurasa 98 iliyopewa kichwa “Ninahitaji Tu Haki: Ukamataji kinyume cha sheria na ukiukwaji wa haki za binadamu magerezaji nchini Uganda,” imeainisha visa vya watu kutoweshwa, kkamatwa kiholela, mateso na dhuluma nyinginezo zinazofanywa na maafisa wa polisi, jeshi, majasusi wa serikali na vyombo vingine vya usalama, hususan katika magereza. Matukio hayo yalifanyika mwaka 2018, 2019 na mwezi Januari wakati wa kipindi cha uchaguzi wa mwaka 2021.

Oryem Nyeko ambaye ni mtafiti katika shirika la Human Rights Watch nchini Uganda amesema serikali ya Uganda imeruhusu visa vya ukamataji kiholela, watu kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria huku maafisa wake wakiwadhulumu wafungwa. Kulingana na Oryem Nyeko, hatua za dharura zinahitajika kuwasaidia waathiriwa, kuwawajibisha maafisa husika na kukomesha kadhia hiyo ya dhuluma na ukiukwaji wa haki kiholela.

Japo wakati mwingine, maafisa wamekiri kutokea dhuluma hizo, hawajafanya ya kutosha kuwapa wahanga na familia zao haki. Wahanga wanazidi kukabiliwa na changamoto za kimwili, kiakili na kiuchumi hata baada ya kuachiwa kutoka magerezani na wanashindwa kupata haki.

Kati ya Aprili 2019 hadi Novemba 2021, shirika la Human Rights Watch liliwahoji watu 51, wakiwemo 31 waliowahi kuwekwa kizuizini, mashahidi wa utekaji na ukamataji w apolisi, maafisa wa serikali, wabunge, wanadiplomasia, wanaharakati na wanahabari mjini Kampala Uganda.

Waliopitia madhila hayo walisema maafisa wa usalama walikiuka kiholela taratibu za kukamata na kuwaweka washukiwa rumande. Kwamba maafisa wa usalama waliwapiga waathiriwa katika maeneo yao ya kazi, nyumbani au mitaani na kuwalazimisha wakati mwingine kwa kuelekezwa bunduki kuingia katika magari yasiyokuwa na namba za usajili. Wakati mwingine wafungwa walipelekwa katika kisiwa kwenye ziwa Victoria, kuzuiliwa kwenye majumba ya chini ya ghorofa au katika kambi za jeshi.

Mnamo Februari 5, 2020, kamati ya Bunge kuhusu haki za binadamu ilitoa ripoti ya uchunguzi wake mwaka uliotangulia kuhusu madai kwamba maafisa w ausalama wa ndani (ISO) waliwateka zaidi ya watu 400 kinyume cha sheria. Ripoti hiyo ilithibitisha kuwa mashirika ya serikali yanayohusika na usalama yalikuwa yakiwashikilia watu katika maeneo yaliyopewa jina ‘safehouses’ nyumba salama. Kamati hiyo ilipendekeza kwamba mashirika husika yachunguze madai hayo zaidi. Lakini serikali haijachukua hatua yoyote kuhusu pendekezo hilo ili kutokeza kadhia hizo.

Miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 2021, na pia miezi kadhaa iliyofuata uchaguzi huo, visa vya ukiukwaji w ahaki za binadamu ziliongezeka. Katika mji wa Kampala na viunga vyake, maafisa wa usalama walikamata watu kiholela na kuwatowesha kwa lazima hasa waliokuwa wakosoaji wa serikali, viongozi wa upinzani, wafuasi wao na waliodaiwa kuandamana. Japo maafisa tayari wameshawaachia huru baadhi ya waliokamatwa, wengine bado hawajulikani waliko hadi leo.

Wafungwa wa zamani wameeleza kwamba maafisa wa usalama waliwanyima haki ya kuwa na mawakili au kuonana na jamaa zao badala yake waliwatesa hata kutumia umeme na kudungwa sindano wasiyojua ina nini. Wafungwa wengine walibakwa na dhuluma nyinginezo za kingono walipokuwa kizuizini.

Maafisa wa usalama waliwatuhumu washukiwa kwa kuwa na njama ya kupanga mauaji dhidi ya maafisa wakuu wa serikali, ujasusi na kupanga njama na washindani wa rais Yoweri Museveni kumuondoa madarakani.

Katika matukio mengi, maafisa wa usalama walipuuza maagizo ya mahakama kutaka wafungwa waachiliwe huru.

Sheria na Uganda nay a kimataifa inapinga kikamilifu visa vya ukamataji w awatu kiholela, kuwatowesha watu kwa lazima na mateso.

(HRW)