1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: uharibifu mkubwa ulifanyika Rakhine

21 Novemba 2016

Shirika la kimataifa la haki za binadamu, la Human Rights Watch, limetoa picha za satelaiti Jumatatu (21.11.2016) zinazoonyesha uharibifu mkubwa kwenye jimbo la Rakhine lililopo nchini Myanmar.

https://p.dw.com/p/2T0FS
Myanmar Konfikte in Rakhine Region
Picha: Reuters/Soe Zeya Tun

Shirika hilo la Human Rights Watch, limetoa mwito kwa Umoja wa Mataifa kuitisha uchunguzi juu ya makabiliano hayo yaliyodumu kwenye eneo hilo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa. 

Kulingana na ripoti ya shirika hilo, nyumba 820 zilizoko katika kijiji cha kabila ya Rohingya, Kaskazini Magharibi mwa Myanmar zimeharibiwa katika makabiliano hayo ya kati ya Novemba 10 na 18, na kufikisha idadi ya nyumba zilizoharibiwa kuwa 1,250. 

"Picha hizi za satelaiti zinazoashiria hali ya hatari zinaonyesha wazi kwamba uharibifu uliofanyika katika vijiji hivyo vya Warohingya na maeneo mengine ni mkubwa zaidi ya kile kilichoelezwa na serikali, amesema Mkurugenzi wa shirika hilo ukanda wa Asia, Brad Adams, kwenye taarifa yake.

"Matukio ya hivi karibuni ya uhalifu na yaliyokusudiwa ya uchomaji wa nyumba dhidi ya vijiji vitano vya kabila ya Rohingya ni matukio yanayoamsha wasiwasi mkubwa, ambao serikali inahitaji kuyafanyia uchunguzi na kuwafungulia mashitaka wahusika wa matukio hayo, amesema mkurugenzi huyo.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, kiasi ya watu 30,000 wameyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi hayo, na nusu kati yao wamekimbia ndani ya siku mbili, wakati ambapo kumetokea vifo vya makumi ya raia baada ya serikali kupeleka helikopta zilizokuwa na silaha. 

Shirika hilo la haki za binaadamu, limeitaka serikali ya Myanmar kuruhusu Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi huru kwenye eneo hilo, linalokaliwa na watu wa Rohingya, ambayo ni kabila ya waumini wa dini ya Kiislamu walio wachache wanaolazimishwa kuishi kwenye makambi huku wakikabiliwa na upungufu mkubwa wa huduma za afya, kazi na elimu.  

Aung San Suu Kyi akabiliwa na ukosoaji mkubwa.

Myanmar Historische Friedenskonferenz
Mshauri mkuu wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka jumuiya ya kimataifa kuhusu hali ya mambo nchini mwake.Picha: picture alliance/AP Photo/Aung Shine Oo

Awali, serikali iliwatuhumu watu wa eneo hilo kuchoma nyumba zao wenyewe kwa nia ya kupata misaada kutoka jumuiya za kimataifa. Makabiliano ya hivi karibuni, yalianza mwanzoni mwa mwezi Octoba baada ya walinzi wawili wa mpakani kushambuliwa na kusababisha vifo vya polisi 9.

Mamia ya watu wa kabila hiyo ya Rohingya ambao kwa muda mrefu wameishi chini ya ukandamizaji wa serikali wamejaribu kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh ili kuepuka mashambulizi hayo. washuhudiaji na wanaharakati wamearifu kwamba majeshi yamekuwa yakiwauwa raia hao, kuwabaka wanawake, kuwaondoa na kuchoma nyumba. Hata hivyo serikali imekataa kuruhusu wachunguzi wa kimataifa kufuatilia hali ilivyo.

Mshauri mkuu wa Myanmar na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi anakabiliwa na ongezeko la shinikizo kutoka jumuiya ya kimataifa la kusuluhisha janga hilo la kibinaadamu nchini humo. Kinyume chake, serikali yenyewe imepinga tuhuma hizo kwa kusema ni sehemu ya kampeni ya kutoa taarifa za uongo inayopandikizwa na iliyowaita "magaidi"

Mmoja wa mawaziri wa serikali ya Myanmar Win Myat Aye aliyetembelea eneo linalokabiliwa na machafuko akiwa na ujumbe uliopeleka misaada ya vyakula ameviambia vyombo vya habari kwamba watoto wote kutoka vijiji vilivyoshambuliwa walikuwa katika afya njema, tofauti na taarifa za chinichini zinazotolewa kwamba wanakabiliwa na upungufu wa lishe.

Kuibuka kwa machafuko magharibi mwa Jimbo la Rakhine, kumeongeza hali ya waiwasi ambayo tayari imesababisha kuongezeka kwa ukosoaji mkubwa dhidi ya mshauri mkuu wa Myanmar, Suu Kyi, ikiwa ni miezi saba tangu uongozi mpya kushika madaraka chini yake. zaidi ya watu 100 wamekufa tangu mwaka 2012 katika makabiliano kati ya waumini wa Buddha walio wengi na Waislamui wa Rohingya walio wachache, wakati ambapo wengi wao wakilazimika kuishi kwenye makambi.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef