HRW yaitaka Eswatini kuheshimu haki za raia
1 Julai 2021Ripoti ya shirika hilo iliyotolewa siku ya Alhamisi imelitaka taifa hilo la kifalme linaloongozwa na Mfalme Mswati wa Tatu, kuzingatia sheria zilizopo na kujiepusha na matumizi ya nguvu kiholela.
Eswatini imetumbukia katika maandamano ya siku tano ya kudai demokrasia yaliyogeuka kuwa ya vurugu. Human Rights Watch imeitaka Eswatini kuhakikisha kwamba vikosi vya usalama vilivyosambazwa kwa ajili ya kukabiliana na maandamano ya umma vinaheshimu haki za raia na kuzingatia viwango vya kimataifa vya utekelezaji wa sheria.
HRW: Raia wanapaswa kulinda
Mkurugenzi wa Human Rights Watch kusini mwa Afrika, Dewa Mavhinga amesema kuwa nchi hiyo inapaswa kuchukua hatua kadhaa za kuwalinda raia dhidi ya ghasia na kuwashitaki wale wote wanaotumia nguvu kinyume cha sheria.
Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu liliwahoji waandamanaji wanane kwa njia ya simu. Walielezea jinsi vikosi vya usalama vilivyowafyatulia risasi waandamanaji kiholela.
Wimbi la maandamano lilianza Mei mwaka huu wa 2021, wakati wanafunzi na walimu walipoandamana kupinga mauaji ya Thabani Nkomonye, yaliyofanywa na polisi. Thabani alikuwa mwanafunzi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Swaziland.
Maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi wa mauaji hayo, lakini maandamano yaliongezeka mwishoni mwa mwezi Juni, ambapo takribani vijana 500 waliingia mitaani katika wilaya ya Manzini, umbali wa kilomita 30 kutoka kwenye mji mkuu, Mbabane, wakidai mageuzi ya kidemokrasia.
Maafisa walijibu kwa kuzuia maandamano na kupeleka wanajeshi na polisi kwa ajili ya kuwatawanya waandamanaji. Kamishna wa taifa wa polisi, William Dlamini, alionya kwamba hawatowavumilia watakaokiuka marufuku hiyo na kile alichokitaja kuwa vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na waandamanaji.
Serikali yataka utulivu
Juni 29, Waziri Mkuu wa Eswatini, Themba Masuku alichapisha taarifa kupitia ukurasa wa Twitter, akitoa wito wa kuwepo utulivu, watu kujizuia na amani itawale. Aidha, alikanusha uvumi kwamba Mfalme Mswati ameikimbia nchi hiyo.
Masuku pia alitoa taarifa inayosema kuwa serikali imesikia kilio cha waandamanaji na alikiri kwamba vikosi vya usalama vilitawanywa mitaani na alitangaza sheria ya kuwazuia watu kutoka nje nchi nzima kati ya saa kumi na mbili jioni na saa kumi na moja asubuhi.
Mahvinga amesema kuwa wimbi jipya la maandamano nchini Eswatini ni tahadhari kwa Mfalme Mswati ambaye ameiongoza nchi hiyo tangu mwaka 1986 na serikali yake kutii wito na kufanya mageuzi. Ameongeza kusema kuwa mshikamano wa kikanda unahitajika ili kuishinikiza Eswatini kuanzisha utamaduni wa uwajibikaji pamoja na kuheshimu haki za binaadamu za watu wote wa taifa hilo.
Human Rights Watch imeitaka jumuia ya kimataifa ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika, SADC kuchangia haraka katika juhudi za kusaidia kufanyika mageuzi ya kidemokrasia na haki za binaadamu nchini Eswatini na kuhakikisha hali ya sasa haiwi mbaya zaidi.
(HWR https://bit.ly/3w3B3a0)