1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yaitaka Nigeria kuwawajibisha wahusika wa mauwaji

Saleh Mwanamilongo
9 Mei 2022

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema mamlaka ya Nigeria haijafanya jitihada zozote kuhakikisha haki inatendeka kwa mauaji ya waandamanaji mwaka 2020.

https://p.dw.com/p/4B1Nx
Nigeria ilikumbwa na maaandamano ya vijana mnamo 2020 wakidai kuvunjwa kwa kikosi maalumu cha polisi cha SARS
Nigeria ilikumbwa na maaandamano ya vijana mnamo 2020 wakidai kuvunjwa kwa kikosi maalumu cha polisi cha SARSPicha: Sunday Alamba/AP/picture alliance

Anitie Ewang, mtafiti wa Nigeria katika shirika la Human Rights Watch anasema ripoti ya jopo la mahakama la uchunguzi haipaswi kufumbiwa macho bila madhara yoyote kwa wale waliohusika na mauaji na kuwajeruhi waandamanaji. Anasema kushindwa kufanyia kazi mapendekezo ya jopo la uchunguzi kutatuma ujumbe mchungu kwa waathiriwa na hatari ya kuhimiza vurugu zaidi kutoka kwa maafisa wa usalama.

Mnamo Oktoba 2020, vijana kote Nigeria waliingia barabarani wakitoa wito wa kuvunjwa kwa kitengo cha polisi kinachojulikana kama Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (SARS) na kukomesha ukatili, katika harakati zilizotumia hashtag (alama ya reli) #EndSARS.

Vikosi vya usalama vilijibu maandamano hayo kwa matumizi ya nguvu, ikiwa ni pamoja na ufyatuaji risasi. Mojawapo ya ukandamizaji mbaya zaidi ulikuwa kwenye eneo la Lekki Toll Gate mjini Lagos mnamo Oktoba 20, wakati maafisa wa jeshi na polisi walipoufyatulia risasi umati wa waandamanaji, na kusababisha watu kadhaa kufa na wengine kujeruhiwa.

Kufuatia tukio hilo, gavana wa jimbo la Lagos, Babajide Sanwolu, aliamuru jopo la mahakama kuendesha uchunguzi na kutoa mapendekezo ya haki na uwajibikaji.

Soma pia→Jeshi liliwauwa waandamanaji Nigeria

Fidia kwa waathiriwa

HRW imeitaka mamlaka ya Nigeria kuwawajibisha wahusika
HRW imeitaka mamlaka ya Nigeria kuwawajibisha wahusikaPicha: PIUS UTOMI EKPEI/AFP/Getty Images

Jopo hilo lifanya uchunguzi kwa mwaka mmoja, kutoka kwa waathiriwa na wawakilishi wa jeshi, polisi, na hospitali zilizowatibu waathiriwa. Ripoti ya jopo iliyotolewa mnamo Novemba 202, iligundua kwamba vikosi vya usalama viliwapiga risasi, kuwajeruhi, na kuwaua waandamanaji wasiokuwa na silaha.

Jopo hilo pia liliwasilisha orodha ya majeruhi wasiopungua 48, wakiwemo tisa waliofariki, wanne waliopotea na wanaodhaniwa kuwa wamekufa, na 21 waliojeruhiwa kwa risasi. Jopo hilo lilipendekeza hatua zinazofaa za kinidhamu, na kufukuzwa kazi kwa maafisa wa jeshi waliohusishwa na unyanyasaji huo.

Jopo hilo pia lilipendekeza kuwashtaki maafisa wa polisi waliohusishwa na kuwapiga risasi kiholela na kuwaua waandamanaji na malipo ya haraka ya fidia kwa waathiriwa.

Soma pia→Nigeria: Mwaka mmoja baada ya maandamo ya #EndSARS

Serikali yatupilia mbali tuhuma za mauwaji

Serikali ya Nigeria, iliyowakilishwa na waziri wa habari, Lai Mohammed, ilikataa matokeo na mapendekezo ya jopo hilo na kusema taarifa za mauwaji ya waandamanaji ni za uongo.

Shirika la Human Rights Watch limesikitishwa kuona miezi sita baada ya uchunguzi huo, polisi wa Nigeria na mamlaka za kijeshi hazijachukua hatua zaidi za kuchunguza kwa uhuru wala kujibu matokeo na mapendekezo ya jopo hilo. Human Rights Watch inasema gavana wa jimbo la Lagos, ambaye alitaka uchunguzi ufanyike na kutoa hakikisho kwamba waathiriwa watafungwa, pia amekuwa kimya kuhusu suala la uwajibikaji.