1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yaituhumu serikali ya Burkina Faso kwa mauaji ya raia 60

25 Januari 2024

Shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Human Rights Watch limeituhumu Burkina Faso kwa kuwaua karibu raia 60 katika shambulizi la droni ambalo serikali imesema lilikuwa linawalenga wanamgambo wa itikadi kali.

https://p.dw.com/p/4bg9a
Burkina Faso
Jeshi la Burkina Faso likirusha droni mwaka 2019.Picha: Dracorius White/ZUMAPRESS/picture alliance

Shirika hilo limesema vifo hivyo vimetokea tangu mwezi Agosti katika mashambulizi matatu ya droni, mawili yaliyofanywa katika soko ambalo hufurika watu na jingine kwenye mazishi.

Limesema liliwahoji mashuhuda kadhaa kati ya mwezi Septemba na Novemba na kuchunguza picha, video na picha za satelaiti na kusema Burkina Faso ilitumia silaha za usahihi kabisa kushambulia makundi ya watu na kusababisha vifo vya raia, ikiwa ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za vita.

Human Rights Watch limeiomba serikali ya Burkina Faso kuchunguza mara moja na bila upendeleo kile kinachoonekana kuwa ni uhalifu huo wa kivita, kuwawajibisha wahusika na kuwasaidia wahanga pamoja na familia zao.