1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yataka Burundi kuwaachilia wahamiaji wanaoshikiliwa

9 Machi 2021

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limezitaka mamlaka za Burundi kutupilia mbali lilichokiita mashtaka yasiyo na msingi na ziwaachilie huru wakimbizi waliorudishwa nchini humo kwa lazima.

https://p.dw.com/p/3qNrF
Burndi Gitega Polizei

Mnamo Februari 26 mwaka huu mahakama ya Muha mjini Bujumbura ilifanya uamuzi wa kutowaachilia wahamiaji hao, licha ya kuwa upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa kuthibitisha haja ya kuendelea kushikiliwa kwa wahamiaji hao. Isitoshe kumekuwa na ukiukwaji wa mara kwa mara wa haki kuhusu mchakato wa kisheria dhidi yao.

Lewis Mudge ambaye ni mkurugenzi mkuu wa Human Rights Watch tawi la Afrika ya Kati, amesema taifa la Burundi linaongeza chumvi kwenye kidonda kwa kushtaki kundi la wahamiaji ambao tayari walifanyiwa jinai na masaibu ya kikatili nchini Tanzania.

HRW: Mashtaka yasiyo na msingi yapaswa kutupiliwa mbali

Ameongeza kwamba mashtaka hayo yasiyo na msingi yanaonesha jinsi kurudishwa kwa wahamiaji hao kumeingiliwa kisiasa na namna gani utawala nchini Burundi ungali unadhibiti mahakama.

Wahamiaji hao wanane wakiwemo Anaclet Nkurunzima na Revocatus Ndayishimiye walikamatwa katika kambi za wakimbizi Mtendeli na Nduta nchini Tanzania kati ya Julai na Agosti mwaka 2020.

Wahamiaji wa Burundi walioko Tanzania waanza kurejea nyumbani

Maafisa wa Tanzania waliwaweka kizuizini katika kituo cha polisi cha Kibondo kwa wiki kadhaa, ambako pia waliteswa.

Wahamiaji wanaoshtakiwa wadai waliteswa

Wahamiaji hao walisema kuwa wakati waliposhikiliwa katika kituo cha polisi cha Kibondo, maafisa wa intelijesia na polisi wa Tanzania waliwadhulumu na kuitisha shilingi milioni moja za Tanzania ndipo waachiliwe huru.

Waliposhindwa kulipa fedha hizo walikabidhiwa kwa maafisa wa mipaka wa Burundi wakiwa wamefungwa pingu mikono na nyuso pia kufunikwa kwa vitambaa.

Wanne kati yao kwa sasa wako katika gereza la Bubanza na wengine wanne wako gereza la Muramvya.

Kesi dhidi yao ilisikizwa mwanzo Februari 24 mwaka huu, ikiwa ni miezi sita tangu majalada yao yalipopelekwa mahakama kuu mnamo Septemba 7.

Wakati wa kusikizwa kwa kesi yao, mmoja kati ya majaji watatu alisema kesi dhidi yao ni ya kisiasa na kwamba upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi kuhusu mashtaka kwamba washukiwa wanashirikiana na makundi yenye silaha na kwamba ni tishio kwa usalama wa taifa.

Rais mpya wa Burundi ataboresha haki za binadamu?

HRW: Mamlaka Burundi zapaswa kuwachunguza maafisa wa polisi

Shirika la Human Rights Watch limeutaka upande wa mwendesha mashtaka kutupilia mbali mashtaka hayo yasiyokuwa na msingi. Badala yake uchunguze matendo ya mamlaka za serikali wakiwemo maafisa wa intelijensia na wa polisi waliowarudisha wahamiaji hao Burundi kwa lazima, kwa ushirikiano na wenzao wa Tanzania.

Sheria ya kimataifa kuhusu haki za kisiasa na umma (ICCPR) ambayo Burundi ilisaini mwaka 1990, inaeleza kwamba watu hawapaswi kuwekwa kizuizini wanaposubiri kesi yao kuanza ila tu kama kuna sharti la hilo ili kuzuia mshukiwa kuhamia nchi nyingine au ili asivuruge ushahidi na pia kumzuia kufanya uhalifu zaidi.

Shirika la Human Rights Watch limesema nchini Burundi, watu wanaotizamwa kuwa wapinzani wakiwemo wahamiaji wanaorudi nyumbani wako katika hatari ya kukandamizwa.

(https://www.hrw.org/news/2020/11/30/tanzania-burundian-refugees-disappeared-tortured)