Hukmu ya Aung San Suu Kyi
10 Agosti 2009Hukmu dhidi ya kiongozi wa upinzani wa Burma,Aung San Suu Kyi inatazamiwa kutangazwa hii leo.Akikutikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka mitano jela.Lakini kuna wanaoamini pengine hukmu hiyo ikaakhirishwa tena kutokana na hali ya afya ya raia wa kimarekani ambae ndie chanzo cha kushtakiwa mshindi huyo wa zawadi ya amani ya Nobel.
Wakizungumza bila ya kutaja majina yao,maafisa kadhaa wa Burma wamesema hali ya John Yettaw,mwanajeshi wa zamani wa kimarekani mwenye umri wa miaka 54,imeanza kuboreka kidogo baada ya kupigwa na kifafa mara tatu hapo awali.Hata hivyo maafisa hao hawakuondowa uwezekano wa kesi hiyo kuakhirishwa kwa mara nyengine tena na angalao kwa wiki moja.
John Yettow,ambae bado amelazwa hospitali,ameanza upya kula baada ya funga ya siku kadhaa tangu alipokamatwa."Ikiwa hali yake haitabadilika kuna uwezekano hukmu ikaakhirishwa" amesema kwa upande wake mwanadiplomasia mmoja wa magharibi.
""Wana upenu wa kati ya Agosti 10 na Agosti 20.Baada ya hapo serikali zitaanza harakati zao za kawaida na kuna mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa unaoweza kugeuka kongamano la kuulaani utawala wa kijeshi" amefafanua mwanadiplomasia huyo.
Kesi ya bibi Aung San Suu Kyi inayokosolewa na kulaaniwa kote ulimwenguni,imeanza tangu May 18 mwaka huu katika ukumbi wa jela moja ya kaskazini mwa mji mkuu Rangun.Vikao vingi vya kesi hiyo vimekua vikiendeshwa kwa siri.
Mshindi huyo wa zawadi ya amani ya Nobel na mshitakiwa mwenzake John Yettaw na washirika wengine wawili wanaoshitakiwa pamoja na kiongozi huyo wa upinzani wa Burma wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka mitano jela wakikutikana na hatia.
Aung San Suu Kyi,mwenye umri wa miaka 64,anatuhumiwa kuvunja sheria za kifungo cha nyumbani,kwa kumkaribisha kwa muda mfupi John Yettow aliyevuka mto kwa kuogelea hadi ndani ya nyumbani ya mshindi huyo wa zawadi ya amani ya Nobel.
Kisa hicho cha ajabu kilifichuliwa na viongozi wa kijeshi wa Burma,wiki tatu kabla ya kumalizika muda wa kifungo cha nyumbani cha Aung San Suu Kyi anaenyimwa uhuru tangu miaka 14 kati ya 20 iliyopita.
Kesi dhidi ya kiongozi huyo wa upinzani wa Burma ni kizungumkuti kikubwa kwa watawala wa kijeshi wanaoshinikizwa na dunia nzima huku wakipania kwa kila hali kumtenga mshindi huyo wa zawadi ya amani na jukwaa la kisiasa kabla ya uchaguzi unaotatanisha unaotazamiwa kuitishwa mwaka ujao.
Jumatano iliyopita,katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon aliwasihi kwa mara nyengine tena watawala wa kijeshi wa Burma wawaachie huru wafungwa wote wa kisiasa na hasa,kama alivyosema "Aung San Suu Kyi."
Ban Ki Moon alisema hayo baada ya mkutano pamoja na kundi la mataifa 14 yanayomunga mkono katibu mkuu wa Umoja wa mataifa katika suala la Myanmar( kama Burma inavyojulikana kirasmi.)
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa anaamini,wachina na warusi wamekua wakizungumza na viongozi wa Burma kuhusu kesi ya Aung San Suu Kyi na kuwaelezea msimamo wa jumuia ya kimataifa.Haijulikani lakini kama majenerali watazingatia maoni ya walimwengu.
Mwandishi:Schilling KLatrin/ZR/O.Hamidou
Mhariri:M.Abdul-Rahman