Hukumu ya kutisha yakosolewa Misri
25 Machi 2014Kesi dhidi ya kiongozi wa kundi la Udugu wa Kiislamu Mohammed Badie na wafuasi 682 wa kundi hilo imekuja siku moja baada ya mahakama hiyo ya mkoa wa Minya kutoa adhabu ya kifo dhidi ya wafuasi wengine 529 wa kundi hilo,hukumu ambayo mashirika ya kutetea haki za binadamu imesema ndiyo ya kwanza ya aina yake kushudiwa katika historia ya Misri,ikilihusisha kundi kubwa la watu.Mawakili wa kundi hilo wanasema watadai kujiuzulu kwa jaji aliyepitisha hukumu hiyo iliyofikiwa baada ya vikao viwili tu vya kuisilikiza kesi dhidi ya kundi hilo la wafuasi wa Udugu wa Kiislamu.
Wataalamu wa masuala ya kisheria hata hivyo wanasema hukumu hiyo huenda ikabatilishwa katika mahakama ya rufaa.Hukumu hiyo iliyotolewa katika kipindi cha muda mfupi ilizusha malalamiko na kukosolewa Kimataifa pamoja na kupigiwa kelele na wapinzani wa serikali iliyowekwa madarakani na jeshi.
Marekani imehoji utendaji wa mahakama hiyo iksema ni vipi mahakama inaweza kusikiliza kesi hiyo kwa njia ya haki ikiwa kesi hiyo imeendeshwa kwa muda wa siku mbili tu?Kesi hiyo ilifunguliwa Jumamosi na Jumatatu hukumu ikatolewa,hatua ambayo Marie Harf msemaji wa naibu waziri wa mambo ya nje,anasema imesababisha wasiwasi mkubwa na kuishutuwa serikali ya mjini Washington.
Halikadhalika Umoja wa Ulaya umepaaza sauti kuikosowa hatua hiyo,mkuu wa sera za nje Catherine Ashton ameutolea mwito Utawala wa Misri kuwatetendea haki washtakiwa katika kesi hiyo.Itakumbukwa kwamba tangu serikali hiyo ilipoingia madarakani imewashtaki zaidi ya wafuasi 2000 wa kundi hilo la Udugu wa kiislamu,baada ya kupinduliwa mwezi Julai rais aliyeingia madarakani kidemokrasia Mohammed Mursi.
Kwa ujumla wafuasi kiasi 1200 wanaoshtakiwa katika mahakama hiyo ya mkoa wa Minya wanatuhumiwa kuhusika na mauaji,jaribio la kuwaua askari kadhaa wakati wa ghasia zilizoibuka mwezi Agosti 14 wakati ambapo polisi ilihusika kuua mamia ya wafuasi wa rais Mursi pale walipozivamia kambi mbili za wafuasi hao kwa lengo la kuwatawanya. Maelfu ya wanachama wa Udugu wa kiislamu walikamatwa na viongozi wa juu wa kundi hilo akiwemo Mursi wanakabiliwa na kesi.Na kama haitoshi serikali ililitangaza kundi hilo kuwa la kigaidi ingawa Udugu huo wa kiislamu unasema umejitolea kutekeleza harakati za amani.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed AbdulRahman