1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUganda

ICC kuthibitisha mashitaka dhidi ya mbabe wa kivita Kony

30 Oktoba 2024

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai - ICC imesema kikao cha kuthibitisha mashitaka dhidi ya mbabe wa kivita anayesakwa Joseph Kony kitafanyika bila yeye kuwepo mahakamani.

https://p.dw.com/p/4mNlk
Lord Resistance Army nchini Uganda
Joseph Kony alianzisha kundi la LRA katika miaka ya 1980 nchini UgandaPicha: Stuart Price/dpa/picture alliance

ICC imesema tarehe ya kusikilizwa hoja hizo itatolewa baadae. Kony mwenye umri wa miaka 63, amekuwa akisakwa na mahakama hiyo yenye makao makuu yake mjini The Hague tangu mwaka 2005.

Soma pia: Mahakama Uganda yamfunga miaka 40 kamanda wa waasi wa LRA kwa uhalifu wa kivita

Anasakwa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu kufuatia miongo mitatu ya ukatili wa kundi lake la waasi wa Lord's Resistance Army - LRA katika mataifa kadhaa ya Kiafrika. ICC ilitangaza miezi sita iliyopita kuwa itafanya vikao mwezi huu wa Oktoba kuthibitisha makosa 36 dhidi ya Kony, ambaye hajulikani aliko kwa sasa.

Kony alianzisha LRA katika miaka ya 1980 na lengo la kuanzisha utawala kwa kuzingatia Amri Kumi za Mungu. Kundi hilo lilianzisha uasi dhidi ya Rais Yoweri Museveni ambao ulisambaa hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan. Liliwauwa zaidi ya watu 100,000 na kuwateka nyara watoto 60,000 waliolazimishwa kuwa watumwa wa ngono, askari na wapagazi.