Idadi ya vifo kutokana na COVID -19 yakaribia 200,000
25 Aprili 2020Serikali duniani zinajaribu kudhibiti msukosuko wa kiuchumi uliosababishwa na virusi vya corona ambapo tayari watu wapatao milioni 2.8 wameambukizwa huku ulimwengu ukishuhudia hatua zinazochukuliwa na serikali mbalimbali zinazowalizimu watu kubakia majumbani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewataka viongozi duniani, mashirika ya kimataifa na sekta binafsi kujiunga na kushirikiana katika juhudi za kutafuta chanjo. Guterres amesema ulimwengu unakabiliwa na kitisho kisicho na mfano.
Wakati wa mkutano uliofanyika kwa njia ya video na kuhudhuriwa na viongozi wa Ufaransa na Ujerumani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza kwamba chanjo salama dhidi ya virusi vya corona inapaswa kuwa nafuu na itakayopatikana kwa wote.
Mlipuko wa virusi vya corona umesababisha ulimwengu kutumbukia kwenye hali mbaya na kukabiliwa na mtikisiko kwenye uchumi wa dunia. Viongozi wa ulimwengu wanajaribu kuyaweka sawa maswala ya afya ya umma na mahitaji ya kiuchumi.
Mbali na Marekani, nchi zingine tayari zimeanza kulegeza vikwazo. Italia imeztangaza kuwa itaanza kulegeza masharti ya kubaki majumbni kuanzia Mei 4. Sri Lanka imesema itaondoa sheria ya kutotoka nje kwa nchi nzima kuanzia Jumatatu baada ya amri hiyo kuwepo kwa zaidi ya wiki tano.
Ubelgiji ndio taifa la hivi karibuni barani Ulaya kutangaza kuwa litalegeza vikwazo vya kubakia majumbani ifikapo katikati ya mwezi Mei.
Katika upande mwingine wa ulimwengu katika nchi za Australia na New Zealand, watu waliadhimisha kumbukumbu ya maveterani wa vita katika siku inayojulikana kama Anzac ndani ya nyumba zao au kwnye nyua zao.
Na mamilioni ya waislamu wameanza mfungo mwezi mtukufu wa Ramadhani katika ya hali ya watu kubakia majumbani wakikabiliwa na marufuku dhidi ya watu kukusanyika kwa ajili ya sala kwenye misikiti na pia mikusanyiko mikubwa ya jadi ambapo familia na marafiki hukusanyika kwa ajili ya kufuturu kila siku.
Mtoa adhana katika Msikiti Mkuu wa mji mtakatifu kwa waislamu wa Makka huko Saudi Arabia, Ali Mulla amesema kwa kawaida msikiti huo mkuu hujaa maelfu ya watu wakati wa Ramadhani, lakini kwa sasa hakuna mtu.
Shirika la afya duniani WHO limesema kuenea kwa COVID-19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona, kunaongeza hatari zingine za kiafya. WHO imeonya kwamba watu zaidi ya 400,000 wanaweza kufa kutokana na ugonjwa wa malaria kwa sababu ya usumbufu uliopo kwa sasa wa usambazaji wa vyandarua pamoja na dawa.
Tarehe 25 mwezi Aprili ni siku ya kimataifa ya Malaria. Shirika la afya duniani WHO limeelezea wasiwasi wake kwamba ugonjwa huo unaweza kusababisha vifo zaidi katika mwaka huu.
Chanzo:/AFP/APE