1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya vifo vya corona yapindukia 290,000 duniani

13 Mei 2020

Janga la virusi vya corona sasa limesababisha zaidi ya vifo 290,000 kote duniani kulingana na idadi ya shirika la habari la AFP. Kati ya mabara yote, Ulaya ndiyo iliyoathirika mno ikiwa na zaidi ya vifo 159,000.

https://p.dw.com/p/3c913
BdTD Italien Turin Patient mit Schnorchelmaske
Picha: AFP/M. Bertorello

Marekani ndiyo nchi iliyo na vifo vingi zaidi duniani, idadi hiyo ikiwa 82,105.

Zaidi ya watu milioni 4.2 wameripotiwa kuambukizwa virusi hivyo kote duniani kwa sasa. Shirika la Afya Duniani WHO lakini limesema kuna matumaini kwa kiasi fulani kwani baadhi ya dawa zinazotumika zinaonyesha kupunguza makali ya ugonjwa wa Covid-19 na kwamba kwa sasa shirika hilo limejikita katika kutaka kufahamu mengi zaidi kuhusiana na dawa nne au tano nzuri zaidi.

Barani Ulaya, idadi ya vifo huko Uingereza kwa sasa vimepindukia 32,000 huku robo ya vifo hivyo vikiripotiwa kutokea katika nyumba za kuwashughulikia wazee. Jambo hili limechangia kwa maswali kuendelea kuzuka kuhusiana na jinsi Waziri Mkuu Boris Johnson anavyolishughulikia janga hili.

Idadi ya maambukizi Ujerumani yashuka na haitarajiwi kupanda tena

Idadi ya vifo Ufaransa iliongezeka kwa 348 Jumanne na kuipiku Uhispania na sasa Ufaransa ndiyo nchi yenye idadi ya nne kubwa zaidi ya vifo duniani baada ya Marekani, Uingereza na Italia.

Präsident Macron | Video Conference
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/Pool/Y. Valat

Nchini Ujerumani idadi ya maambukizi imeshuka chini ya kiwango muhimu cha moja, huku uongozi ukisema hautarajii kuongezeka tena kwa kiwango hicho. Huko Urusi nako licha ya idadi ya maambukizi kuongezeka pakubwa Rais Vladimir Putin ameagiza kulegezwa taratibu kwa vikwazo huku wafanyakazi wa viwanda na ujenzi wakitarajiwa kurudi makazini. Wakati huo huo msemaji wa Rais Putin, Dmitry Peskov amesema ameambukizwa virusi hivyo na kwa sasa anapokea matibabu hospitali.

Nchini Marekani, mtaalam mkuu wa magonjwa ya kuambukiza Anthony Fauci amelionya bunge la congress kwamba kuondoa vikwazo mapema huenda kukasababisha miripuko mingine ya maambukizi ya virusi vya corona ambavyo vimewauwa zaidi ya watu 80,000 nchini humo. Fauci lakini amesema idadi hiyo ya vifo ni ndogo kuliko hali halisi ilivyo.

Serikali ya India itatoa mabilioni ya dola kuufufua uchumi

"Huenda ikawa kuna watu walifariki majumbani na walikuwa na ugonjwa wa Covid na hawakuhesabiwa kwasababu hawakufika hospitali, kwa hiyo, huenda ikawa idadi iko juu zaidi, sijui kwa asilimia ngapi ila iko juu bila shaka," alisema Fauci.

Anthony Fauci USA NIAID 16.10.2014
Mtaalam mkuu wa magonjwa ya kuambukiza Marekani, Anthony FauciPicha: Nicholas Kamm/AFP/Getty Images

Huko barani Asia, maafisa wa afya China wametaka kuwepo na umakini kwani kuna visa vipya vya maambukizi vinavyoshuhudiwa ingawa kilele cha virusi vya corona kimeshapita nchini humo.

Naye Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesema serikali yake itatoa dola bilioni 226 ili kuufufua uchumi wa nchi hiyo uliodorora kutokana na vikwazo vya wiki kadhaa.

Saudi Arabia nayo kupitia kwa waziri wake wa usalama wa ndani imesema itaweka vikwazo vya kutotoka nje kwa saa ishirini na nne kwa siku tano wakati wa sikukuu ya Eid ul-Fitr baadae mwezi huu ili kuzuia maambukizi.

Na barani Afrika Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema itakuwa ni makosa kuandaa uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika mapema mwakani endapo janga la virusi vya corona litaendelea.

Nalo Shirika la Fedha Duniani IMF limeongeza kiwango cha Kenya kulemewa na mzigo wa kulipa madeni yake kutoka kiwango cha wastani hadi cha juu zaidi, kutokana na athari ya virusi vya corona.