Idadi ya vifo yapindukia 17,000 baada ya tetemeko la ardhi
9 Februari 2023Waokoaji wamewavuta manusura zaidi kutoka chini ya vifusi vya majengo yaliyoporomoka lakini matumaini ya kuwapata manusura wengine yanaendelea kudidimia. Kulingana na shirika la AFAD, zaidi ya maafisa wa uokoaji laki moja na elfu kumi sasa wanashiriki katika juhudi hizo za uokoaji na zaidi ya magari 5,500 yakijumuisha matrekta na matingatinga yameelekea nchini humo.
Hata hivyo, kazi hiyo ni kubwa baada ya maelfu ya majengo kuporomoka kutokana na tetemeko hilo la ardhi. Makundi ya waokoaji kutoka zaidi ya nchi 12 yamejiunga na maafisa wa Uturuki wa kukabiliana na hali za dharura katika juhudi hizo za uokoaji, lakini kiwango cha uharibifu kutokana na tetemeko hilo ardhi kilikuwa kikubwa mno na kuenea katika eneo kubwa ambapo watu wengi bado wanasubiri msaada.
Maelfu ya watu wapoteza makazi Antakya
Maelfu ya watu wanaaminika kupoteza makazi yao. Katika jimbo la Antakya, waliokuwa wakaazi wa jengo lililoporomoka, walikusanyika nje katika moto waliowasha usiku kucha hapo jana wakiwa wamejifunika mablanketi kujaribu kujikinga kutokana na baridi kali.
Rais Recep Tayyip Erdogan Alhamisi (9.02.2023) anatarajiwa kuzuru maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo kubwa la ardhi katika mikoa ya Gaziantep, Osmaniye na Kilis wakati ambapo shutuma zinaendelea kutolewa dhidi ya serikali kutokana na kasi ndogo ya kushughulikia janga hilo. Wataalamu wanasema kuwa matumaini ya kupata manusura zaidi ambao bado wamekwama chini ya vifusi yanaendelea kufifia ingawa wanaonya kuwa ni mapema mno kukata tamaa.
Mtandao wa twitter waanza kutumika tena
Haya yanajiri wakati watumiaji wa mtandao wa Twitter nchini Uturuki wakianza kutumia tena huduma hiyo baada ya kuripotiwa vikwazo vya ndani baada ya tetemeko hilo la ardhi mwanzoni mwa wiki. Huduma hizo za mtandao wa Twitter, zimeanza kutumika tena bila ya kutumia huduma za kuwezesha ufikiaji wa mbali wa mtandao huo ama mtandao wa kibinafsi wa VPN. Shirika la Netblocks, linalofuatilia vikwazo vya mtandao, Jumatano (9.02.2023) liliripoti hatua hiyo ya kufungia mtandao na kutaja kuweko kwa huduma nyingi za mtandao nchini Uturuki. Wakati huo, watumiaji wa mtandao huo, waliweza tu kuufikia kwa kutumia huduma ya VPN. Hakukuwa na thibitisho rasmi la awali kuhusu madai hayo ya vikwazo. Wanasiasa na watu maarufu nchini Uturuki, walikuwa wameishtumu serikali ya nchi hiyo kwa kukatiza kwa makusudi mawasiliano kupitia mtandao wa twitter.
Hapo jana usiku, mkurugenzi mkuu wa Twitter, Elon Musk, aliandika ujumbe akisema kuwa kampuni hiyo imepata taarifa kutoka kwa serikali ya Uturuki kwamba huduma hiyo itaanza kutumika tena baada ya muda mfupi. Katika siku chache zilizopita, watu waliokuwa wamefukiwa chini ya vifusi, walitumia mtandao wa kijamii kuomba msaada.