Idadi ya wahanga wa mabomu ya Istanbul yafikia 17 na wengine 154 wajeruhiwa
28 Julai 2008Idadi ya watu waliokufa kutokana na milipuko miwili ya mabomu ya mjini Istanbul Uturuki imepanda kufikia 17 baada ya moja wa majeruhi 150 na ushei kufariki jumatatu asubuhi.
Taarifa za kuongezeka kwa idadi ya vifo zimekuja wakati mahakama moja ya nchini humo ikianza kusikiliza mijadala ya aidha kukipiga marufuku au laa chama tawala nchini humo.
Shirika moja la habari nchini Uturuki la Anatolia,limemnukuu waziri wa afya Recep Akdag akisema kuwa mtu mmoja miongoni mwa wale zaidi ya 150 waliojeruhiwa jana jumapili ameaga dunia.Aidha amesema kuwa idadi inaweza ikapanda wakati wowote kwani wengine saba ambao walijeruhiwa vibaya wako mahtuti.Ameongeza kuwa miongoni mwa waliokufa ni watoto.
Shirika la habari la Anatolia linasema kuwa takriban watu 115 wanatibiwa katika vituo mbalimbali vya kiutibabu katika mji huo.Milipuko hiyo ilitokea jumapili jioni moja baada ya mwingine.Mlipuko wa pili ulitokea dakika kumi baadae.
Habari zinaeleza kuwa mlipuko wa kwanza uliokuwa mdogo kaisi ulitokea katika eneo moja la takataka katika mtaa wa Gungoren unapatikana katika mji wa Istanbul.Mlipuko huo ukavuta umati wa watu waliotaka kuona kilitokea.Na ndipo hapo mlipuko mwingine mkubwa ukatokea mita chache kutoka hapo.
Ndio hapo watu kadhaa wakafariki na wengine kujeruhiwa.Gavana wa eneo hilo Muammer Guler amewambia maripota kuwa bila shaka hicho ni kitendo cha ugaidi ,ingwa hadi kufikia sasa hakuna kundi lolote lililojitokeza kukiri kuhusika.Hata hivyo wakuu wa Uturuki wanawanyooshea kidole wapiganaji wa kundi la Kurdistan Worker's party PKK .
Ofisi ya Gavana ilisema kuwa watu 154 ndio walijeruhiwa.Nae afisa wa serikali aliekuwa katika sehemu ya tukio alisema kuwa kati ya hao wote waliojeruhiwa 15 walikuwa wamejeruhiwa vibaya sana.
Gazeti moja linasema kuwa polisi imewatia mbaroni vijana watatu kuhusiana na milipuko hiyo.
Gazeti hilo la Milliyet linasema kuwa vijana hao wenye umri kati ya miaka 16 na 17 walikamatwa wakiwa wamejificha katika moja wa vyumba vya chini vya jengo moja la karibu na hapo.
Gazeti linaongeza kuwa vijana hao walidai eti walijificha huko kwa kuogopa milipuko.
Shambulio hilo limelaaniwa na wadau kadhaa wa kigeni.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier,akiwa Mazar-e Sharif nchini Afghanistan kwa ziara rasmi ameliita shambulio hilo kama la kigaidi na kuongeza kuwa Ujerumani iko nyuma ya Uturuki.
Nae katibu mkuu wa NATO Jaap de Hoop,akipinga shambulio hilo amesema kuwa NATO daima itasimama kidete na wananchi wa Uturuki katika vita dhidi ya ugaidi.
Haya yote yanakuja wakati mahakama ya juu ya masuala ya kikatiba ikiwa inaaza mjadala muhimu kuhusu mustakabala wa siasa wa nchi hiyo.Mijadala inahusu ikiwa chama tawala cha Justice and Development kipigwe marufu au laa.Kisa na mkasa ni kuwa chama hicho kinaonekana kinakwenda kinyume na utawala wa kutoihusisha serikali katika masuala ya dini.
Mwendesha mashtaka mkuu wa nchi hiyo mwezi wa Machi aliiomba mahakama hiyo kukipiga marufuku chama cha waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan na yeye waziri mkuu mwenyewe kutoshiriki katika masuala ya kisiasa pamoja na wenzake wengine 70 kwa kipindi cha miaka mitano.
Rais wa nchi hiyo Abdul Gul pia naye yuko katika orodha ya mwendesha mashataka mkuu.
Kesi hiyo inaonyesha pengo liliopo kati ya wale wasiopendelea dini kuingizwa katika siasa na chama tawala ambacho wanachama wake wengi ni watu wa dini sana ambao wanauhusiano wa karibu na makundi ya kiislamu.