1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAsia

Idadi ya waliokufa kwa kimbunga yafikia watu 200

Angela Mdungu
12 Septemba 2024

Zaidi ya watu 200 wamefariki dunia nchini Vietnam kutokana na kimbunga Yagi kilichosababisha mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi. Watu wengine 800 wamejeruhiwa kutokana na mkasa huo.

https://p.dw.com/p/4kXcS
Vietnam | Kimbunga Yagi
Kimbunga Yagi kikiwa kinapiga baadhi ya maeneo ya Vietnam.Picha: Nhac Nguyen/AFP/Getty Images

Takwimu za serikali zilizotolewa leo Alhamisi zinaonesha kuwa watu wengine zaidi ya 120 hawajulikani waliko. Maafisa wa kukabiliana na majanga chini ya Wizara ya Kilimo ya Vietnam wamesema kimbunga hicho kilichotokea Jumamosi, kimesababisha pia uharibifu wa zaidi ya hekta 250,000 za mazao. 

Soma pia:Maporomoko ya ardhi na mafuriko yauwa watu takriban 143 nchini Vietnam

Hadi sasa bado maeneo kadhaa yamefunikwa na maji huku maelfu ya watu wakilazimika kuyahama makazi yao. 

Kimbunga Yagi kinatajwa na wataalamu wa hali ya hewa kuwa kibaya zaidi kupiga kaskazini mwa Vietnam kwa miaka 30. Kimesababisha pia madaraja kuvunjika, uharibifu wa majengo na viwanda na kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo.