Idadi ya waliokufa kwa tsunami huko Samoa yaongezeka
30 Septemba 2009Imethibitika kuwa idadi ya watu waliouawa kutokana na tetemeko la ardhi chini ya bahari na hivyo kutokea tsunami katika eneo la Kusini mwa Bahari ya Pacific, imepanda na kufikia 75. Maafisa wamesema watu 47 wameuawa katika kisiwa cha Samoa na 22 katika eneo la karibu la Samoa ya Marekani na watu sita pia katika eneo la karibu la Tonga.
Watu kadhaa hawajulikani walipo na wengine wanahofiwa kufa, lakini maafisa katika visiwa hivyo vitatu vya Kusini mwa Bahari ya Pacific wamesema hakuna mawasiliano na maeneo mengi ya mbali ya vijijini. Katibu wa habari katika ofisi ya waziri mkuu ya Apia, amesema katika taarifa fupi kuwa watu 47 wamethibitika kufa. Russell Hunter, mhariri wa gazeti la Samoa Obsever, amesema idadi ya watu waliokufa inaweza ikaongezeka. Hunter amesema kuna watu wengine wengi katika vijiji na inawezekana idadi hiyo ikaongezeka na kufikia 100 au hata zaidi ya hapo.
Huko Samoa ya Marekani, kiasi kilometa 100 kutoka kisiwa cha Samoa, Mkurugenzi wa Usalama wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Michael Sala, amesema tsunami ambayo ilifuata dakika 20 baada ya kutokea tetemeko hilo la ardhi, imesababisha uharibifu mkubwa. Sala amesema wamethibitisha kuwa watu 22 wamekufa na idadi hiyo inaweza ikaongezeka. Eneo la mashariki la Samoa ya Marekani lilikuwa halina umeme na huduma ya maji baada ya kutokea tetemeko hilo. Aidha, maafisa katika eneo la Tonga wamesema watu sita wamekufa na wanne katika kisiwa kidogo cha Niuatoputapu hawajulikani walipo.
Ukubwa wa tetemeko na wasemavyao viongozi
Kufuatia tetemeko hilo la ardhi chini ya bahari lililokuwa na ukubwa wa 8.0 katika kipimo cha Richter, Rais Barack Obama wa Marekani ametangaza janga kubwa katika kisiwa cha Samoa ya Marekani. Naye Waziri Mkuu wa Samoa, Tuilaepa Sailele Malielegaoi, amesema ameshtushwa sana na tetemeko hilo ambalo hakulitegemea. Waziri mkuu huyo amesema uharibifu mkubwa umetokea na watu wengi wamekufa na wengine hawajulikani walipo. Naye Gavana wa Samoa ya Marekani Togiala Tulafono anasema mawimbi ya tsunami yamesababisha ugumu wa kuwaokoa watu walioko kwenye maeneo yaliyoharibiwa kufuatia kuvunjika kwa daraja. zaidi Gavana Tulafono anasema:
''Kwa mujibu wa watu walioshuhudia, wamesema yalitokea mawimbi manne. Mawimbi ya mara ya pili na mara ya tatu ndiyo yalikuwa yenye nguvu zaidi.''
Wakati huo huo, eneo la pwani ya Japan imekumbwa na mawimbi madogo ya tsunami. Shirika la hali ya hewa limesema mawimbi hayo yamekikumba kisiwa cha kusini mwa Tokyo na kisiwa cha Honshu. Awali shirika hilo lilionya kuwa mawimbi ya tsunami yanaweza yakaikumba pwani ya Japan.
Raia wa nchi nyingine walioathiriwa na tsunami
Nazo taarifa kutoka nchini Australia zinaeleza kuwa raia wawili wa nchi hiyo, akiwemo msichana mwenye umri wa miaka sita, ni miongoni mwa watu waliuawa na tetemeko hilo la ardhi katika kisiwa cha Samoa. Waziri Mkuu wa Australia, Kevin Rudd, ameeleza vifo vya msichana huyo pamoja na mwanamke mwenye umri wa miaka 50 kuwa ni vya huzuni. Raia wengine watatu wa Australia wamelazwa hospitalini baada ya kujeruhiwa katika tetemeko hilo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Australia amesema kikundi cha maafisa wa nchi hiyo kitapelekwa Samoa kutoa msaada baada ya nchi hiyo kuomba msaada, ukiwemo ule wa matibabu, mahema, machera na eneo la muda la kuhifadhia maiti.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)
Mhariri: Miraji Othman