1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya watoto wanaoomba Uganda haipungui

12 Juni 2020

Licha ya juhudi za kuwaondoa watoto wanaombaomba kwenye barabara za miji nchini Uganda, idadi ya watoto hao hasa kutokea eneo la Karamoja kaskazini mashariki mwa Uganda haipungui.

https://p.dw.com/p/3dhRN
Nigeria Kinder
Picha: Imago Images/Zuma

Imebainika kuwa chanzo cha hali hii ni mienendo ya watu wanaoshiriki biashara ya kuwatorosha watu ndani ya nchi. Watu hao huwahadaa wazazi wa watoto hao na kuwaleta mijini ili wawatumikishe kuombaomba.

Halmashauri ya mji wa Kampala KCCA pamoja na wizara inayoshughulikia masuala ya watoto mara nyingi huendesha operesheni za kuwaondoa watoto wanaombaomba kwenye barabara za miji. Lakini kushangaza ni kwamba hawajawahi kufaulu kwa kiasi kikubwa kuwaondoa watoto hao. Kama anavyotamka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka18 anayetokea eneo la Karamoja, wao hudumu katika mchezo wa paka na panya na askari wa halmashauri ya mji KCCA

Halmashauri hiyo ililazimika kuchunguza vyanzo vya watoto hao kuacha familia zao zaidi ya kilomita 800 na jinsi wanavyofika katika mji wa Kampala na mingineo. Kumbe watoto hao walio na umri wa kati ya mwaka mmoja na miaka 25 huuzwa na wazazi na jamaa zao kwa watu wanaowaleta na kuwatumikisha kuomba kwenye barabara za mji.

"Kuna watu wazima ambao tunaweza kuwaita wavunjaji sheria wanaochukua watoto hao kutoka kwa jamaa zao wakiwahidi maisha bora na elimu mjini Kampala lakini wakifika wanawapanga barabarani kuombaomba kwa niaba ya matajiri wao,” alisema msemaji wa halmashauri ya mji wa Kampala, Peter Kauju.

Wenye ushawishi mkubwa ndiyo wanaendesha biashara hii

Biashara hii ya kuwatumikisha watoto kuombaomba inadaiwa kuendeshwa na watu walio na ushawishi mkubwa miongoni mwa vyombo vya kisheria. Ndiyo maana juhudi za asasi mbalimbali kuwakamata watu hao wanaoendesha utoroshaji wa watu ndani ya nchi hazijazaa matunda. Jessica Abenakyo ni meneja wa mawasiliano na mikakati katika shirika la Dwelling Places linalosaidia kuwatunza watoto waliogunduliwa kutoroshwa na kisha kuwarudisha kwa familia zao.

"Watoto hawa huagizwa kukusanya kiasi fulani. Wanatakiwa kukusanya shilingi elfu ishirini za Uganda kila siku. Mara tu unapowapa pesa kiganjani mtu mzima huja na kuzichukua pesa hizo,” alisema Abenakyo.

Utoroshaji huu wa watoto kutoka Karamoja hauishii tu katika kuwatumikisha kuombaomba. Baadhi ya watoto hutolewa na wazazi na jamaa zao kuja kufanya kazi za nyumbani ambapo wao ndiyo hupokea pesa kila mwisho wa mwezi.

"Wengine hugeuzwa kuwa makahaba watoto na kunyanyaswa katika madanguro tena kumbuka wana shida ya lugha,” alifafanua Abenakyo.

Ili kukabiliana na hali hii ya utoroshaji wa watoto,wanaharakati wa haki za watoto wanatoa mwito hali ya maisha iboreshwe katika eneo la Karamoja. Hii ni kwa sababu umasikini wa kipato ndiyo huwasukuma wazazi kuwatoa watoto wao kwa watu wanaowahadaa kuwa watawatunza vyema na kuwapa elimu bora mijini.

Halmashauri ya KCCA ilitunga sheria kumkamata mtu anayetoa pesa kwa watoto hao kama njia mojawapo ya kukomesha biashara hiyo haramu ya kuwatumikisha watoto hao. Lakini wengi hawaitilii maanani kwa kuwaonea huruma watoto hao.