IFAB yaruhusu wachezaji 5 wa akiba
8 Mei 2020Waandaaji wa mashindano ya soka wanaweza kuamua kuruhusu kubadilisha wachezaji watano wa akiba katika kila mechi baada ya idhini kutolewa kwa na Bodi ya kimataifa ya mashirikisho ya soka, IFAB.
Pendekezo hilo lilitolewa na shirikisho la soka ulimwenguni, FIFA kuyalinda masilahi ya wachezaji wakati wa ratiba ya mechi nyingi huku mechi za kandanda zikirejea tena kufuatia janga la virusi vya corona.
Mashindano yaliyopangwa kukamilika hadi kufikia Desemba 31 mwaka 2020 yanaruhusiwa kuiongeza idadi ya wachezaji watatu wa akiba wanaoruhusiwa hivi sasa.
Shirikisho la FIFA na bodi ya IFAB pia wanatazingatia kuirefusha sheria hiyo hadi mwishoni mwa mwaka 2021. Huku timu zikiruhusiwa kubadilisha wachezaji watano, hili sharti lifanyike katika awamu tatu au katika kipindi cha mapumziko ili kulinda mtitiriko wa mchezo.
Shirikisho la soka la Uhispania awali lilisema lingeitumia sheria hiyo kama ingeidhinishwa na ligi ya kandanda ya Ujerumani, Bundesliga, pia itatafakari kufanya mabadiliko hayo. "Kama mchezo utasitishwa mara tatu kwa kila timu, naona ni suluhisho zuri," alisema mkurugenzi wa michezo wa timu ya Bundesliga, Schalke 04, Joachen Schneider.
Shirikisho la soka ulimwenguni FIFA limesema mashindano yanayotumia mfumo wa refarii wa video, VAR, yanaruhusiwa kuacha kuutumia ligi zitakaporejea tena uwanjani.
(dpa)