IGAD yatoa wito wa mazungumzo kutuliza wasiwasi Sudan Kusini
10 Agosti 2021Shirika la Maendeleo la eneo la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD limeyatolea wito makundi yanayohasimiana ya makamu wa rais wa Sudan Kusini Riek Machar yafungue mlango wa kufanyika mdahalo kufuatia mapigano makali ya umwagaji damu yaliyotokea mwishoni mwa juma lililopita. Mataifa ya IGAD yanataka mazungumzo kwa lengo la kupunguza hali ya wasiwasi na machafuko nchini humo.
Shirika la IGAD liliitisha mkutano wa dharura wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama, likisema hali ya sasa ya kisiasa Sudan kusini inahitaji kushughulikiwa kwa dharura na baraza lake.
Soma zaidi: Kiir na Machar waahidi amani na maendeleo Sudan Kusini
Katibu Mtendaji wa IGAD Workneh Gebeyehu amesema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba ameyataka makundi yanayopigana Sudan Kusini yasuluhishe tofauti zao kwa amani.
Gebeyehu amesema amewataka viongozi wa SPLM/SPLA-IO waandae mazingira ya kufanya mdahalo wa kufanya mazungumzo yatakayoleta tija ili kulinda na kuendeleza utekelezaji wa mkataba wa amani uliofanikiwa hapo kabla unaonuiwa kuutanzua mgogoro wa Sudan Kusini.
IGAD imesema hali ya sasa ya Sudan kusini inahitaji kushughulikiwa kwa dharura
Aristes Kabendera, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Kimataifa mjini Dar es Salaam na Mchambuzi wa masuala ya Diplomasia na usuluhishi wa migogoro ya kimataifa, amesema "Tunapozungumzia diplomasia, kuna kitu kinaitwa diplomasia laini na diplomasia nzito. Kwenye diplomasia nyepesi, mutakaa kwenye meza ya mazungumzo ili kujadiliana. Hilo halina mjadala. Katika kujadiliana, ndio munaweka matatizo yenu mezani na kuangalia ni kwa namna gani mutaweza kuyamaliza ikiwa kwenye meza ya mduara, haina mbadala."
Shirika la IGAD limekuwa mdau muhimu katika mazungumzo ya amani yenye lengo la kuvifikisha mwisho vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu muda wa miaka mitano kati ya vikosi vitiifu kwa Machar na hasimu wake wa zamani rais Salva Kiir, ambavyo vimesababisha vifo vya watu takriban 400,000.
Aristedes Kabendera anaelezea kwa nini mgogoro wa Sudan Kusini umekuwa ukijirudiarudia.
"Huu mgogoro unajirudiarudia kwa sababu tunauita mgogoro wa kikorofi lakini jitihadi bado zinaendelea. Ndani ya IGAD, ni mfumo halisi ambao baraza la kimataifa la usalama limewekeza kwamba huu mgogoro uweze kutatuliwa katika ngazi ya kikakanda.Hizi juhudi zinafaa kuendelea na hatimaye zitafanikiwa."
Mivutano na mapigano ndani ya vuguvugu la Machar yanatishia kuongeza shinikizo kwa mkataba ambao tayari unasuasua, uliosainiwa na Machar na Kiir mnamo 2018 na makubaliano yao ya kugawana madaraka. Kila upande unaulaumu mwingine kwa kuanzisha mashambulizi ya alfajiri Jumamosi iliyopita katika jimbo la Upper Nile linalopaka na Sudan.
Msemaji wa kitengo ha kijeshi upande wa Machar amesema vikosi vya Machar viliwaua maafisa wawili wa jeshi wenye cheo cha meja jenerali na zaidi ya wanajeshi 27 adui, na kupoteza wapiganaji wao watatu.
Kwa kujibu hujuma hiyo, vikosi vilivyoongozwa na Simon Gatwech Dual, jenerali aliyetajwa wiki iliyopita kama mkuu wa mpito wa SPLA-IO, alidai kwenye taarifa kwamba walifanikiwa kuwaua wapiganaji 28 adui na wakapoteza wapiganaji wao wanne.
Sudan Kusini imekuwa ikikabiliwa na vita, njaa na mzozo sugu wa kisiasa na kiuchumi tangu ilipopata uhuru wake kutoka kwa Sudan mnamo Julai 2011. Shirika la IGAD linazijumuisha Djibouti, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda. Eritrea ilisitisha uanachama wake wa IGAD 2007 na haijaruhusiwa tena kujiunga na shirika hilo.