1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Infantino rais mpya FIFA

Admin.WagnerD27 Februari 2016

Gianni Infantino alipata ushindi adimu jana Ijumaa na kuchukua wadhifa wa urais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA, na kutoa wito wa mwanzo mpya katika shirikisho hilo baada ya kukumbwa na akashfa kadhaa za rushwa.

https://p.dw.com/p/1I3G0
Schweiz FIFA Gianni Infantino
Gianni Infantino rais mpya wa FIFAPicha: Getty Images/M. Hangst

"Naamini enzi mpya inaanza," alisema Infantino, ambaye amekuwa mgombea mara tu kesi ya kuenda kinyume na maadili ya kifedha ilipomuondoa bosi wake katika shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA , Michel Platini, pamoja na rais anayeondoka madarakani wa FIFA Sepp Blatter.

Infantino aliahidi kukutana haraka na mashirika yanayotangaza kombe la dunia pamoja na wafadhili, akisema "wanahitaji kupata imani na kujiamini katika soka pamoja na ndani ya FIFA.

Schweiz Neuer FIFA Präsident Gianni Infantino
Gianni InfantinoPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Infantino mwenye umri wa miaka 45, mwanasheria wa zamani kutoka Uswisi alipanda na kufikia katika wadhifa huo mkubwa duniani katika soka baada ya hatua za uchaguzi zilizokuwa na mvutano mkubwa uliochukua masaa sita na ushei kumpata mrithi wa kiti kilichokuwa kinashikiliwa na Sepp Blatter.

UEFA-Präsident Michel Platini
Michel PlatiniPicha: picture-alliance/dpa/W. Bieri

Tutarejesha hadhi ya FIFA na heshima ya FIFA. Na kila mtu duniani atatushangiria," amesema Infantino, akimaanisha kuhusu uchunguzi wa rushwa na ufisadi ambao umelitikisa shirikisho hilo linaloongoza kandanda duniani na kumlazimisha Blatter kuachia madaraka baada ya zaidi ya miaka 17 katika uongozi akiwa kama rais.

Infantino , katibu mkuu wa UEFA, ni rais wa pili kutoka katika jimbo la Valais katika milima ya Alps nchini Uswisi. Infantino anatokea Brig na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Blatter mwenye umri wa miaka 79, ambaye ni mzaliwa wa mji jirani wa Visp.

Infantino alizungumza kwa ufupi kuhusu mipango yake ya kurejesha hadhi katika shirikisho hilo.

Amesema kitu cha kwanza kukifanya ni kumtafuta katibu mkuu , akisisitiza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni kwamba hatamchagua mtu kutoka bara la Ulaya, uamuzi wenye lengo la kujenga uwiano wa kikanda katika utawala wa mchezo huo duniani.

FIFA President Sepp Blatter im TV Interview
Sepp BlatterPicha: picture-alliance/dpa/Screenshot Via Keystone

Mgombea aliyeshindwa Sheikh Salman bin Ebrahim Al Khalifa amemwambia rais mpya wa FIFA kwamba bara la Asia linaweza kuwa kutoa mwanga katika njia kwa ajili ya shirikisho hilo la dunia "kurejesha imani katika mchezo wa kandanda".

Sepp Blatter rais wa zamani wa shirikisho hilo amempongeza Gianni Infantino kwa kuchaguliwa kwake kama mrithi wa kiti cha rais wa FIFA kufuatia kampeni iliyolenga katika haja ya kushutumu enzi ya miaka 18 ya utawala wake iliyogubikwa na kashfa tele.

FIFA Kandidat Prinz Ali bin al Hussein
Mwanamfalme Ali bin al-Hussein mgombea mwingine wa kiti hichoPicha: Getty Images/AFP/M. Bradley

Rais wa Urusi Vladimir Putin nae amempongeza Gianni Infantino kwa kuchaguliwa kuwa rais wa FIFA na kuanhidi kusaidiana nae kuhusiana na hali ya wasi wasi inayozunguka Urusi kuwa mwenyeji wa mashindano ya fainali za kombe la dunia mwaka 2018.

Hatua za kuwania kuwa wenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka 2018 , pamoja na zile zitakazofanyika nchini Qatar mwaka 2022, zimeingia katika kurunzi kama sehemu ya uchunguzi wa Marekani na Uswisi katika FIFA.


Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe/ape