1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran haijaalikwa mkutano wa amani Syria

Admin.WagnerD7 Januari 2014

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon siku ya Jumatatu alituma barua za mualiko kwa mataifa 30 yatakayohudhuria mkutano wa amani wa Syria nchini Uswisi mwezi huu, lakini Iran haikuwa miongoni mwa waalikwa.

https://p.dw.com/p/1AmEg
Kikao cha maandalizi ya mkutano wa Geneva II.
Kikao cha maandalizi ya mkutano wa Geneva II.Picha: Getty Images

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, alisema mawaziri wa mambo ya kigeni wa Marekani na Urusi watakuna Januari 13 kuamua juu ya jukumu la Iran katika kukomesha mgogoro wa Syria uliodumu kwa karibu miaka mitatu sasa.

Urusi inaunga mkono ushiriki wa Iran, ambayo inamuunga mkono rais wa Syria Bashar Al-Assad, katika mazungumzo yaliyopangwa kuanza nchini Uswisi Januari 22.

Marekani na mataifa mengine ya magharibi yanasema Iran lazima kwanza iunge mkono tamko la mataifa makubwa la mwaka 2012, linalotaka kuundwa kwa serikali ya mpito nchini Syria, kabla ya kupewa jukumu lolote muhimu katika mazungumzo ya amani.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon jana Jumatatu alituma barua za mialiko kwa mataifa 30 yatakayohudhuria mkutano wa amani wa Syria baadaye mwezi huu, lakini Iran haikuwa miongoni mwao.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.Picha: AP

Jukumu la Iran ni moja ya vizingiti vikubwa ambavyo amekabiliana navyo mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu, Lakhdar Brahimi, katika maadalizi ya mkutano huo wa amani.

Vizingiti bado vingi
Muundo wa ujumbe wa upinzani na ule wa serikali katika mazungumzo hayo pia umesababisha msuguano, na taarifa zaidi za wawakilishi wa pande hizo bado hazijatolewa.

Lakini Msemaji wa Umoja wa Mataifa aliwaambia waandishi wa habari kuwa Ban ameanza kuyaomba mataifa yashiriki, huku akiongeza kuwa Iran haikuwa miongoni mwa waalikwa wa kwanza.

Mataifa 30 yaliyoko katika orodha ya kwanza ni pamoja na Saudi Arabia, ambayo ni muungaji mkono mkubwa wa waasi, pamoja na Uingereza, China, Urusi, Ufaransa na Marekani -- wananchama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa-- na majirani wa Syria kama vile Uturuki, Iraq na Jordan.

Akizungumzia mkutano wa Januari 13 kati ya mawaziri John Kerry na Sergei Lavrov, msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema kuna matumaini makubwa kwamba watafikia makubaliano juu ya ushiriki wa Iran.

Mjumbe maalumu wa kimataifa kuhusu Syria Lakhdar Brahimi.
Mjumbe maalumu wa kimataifa kuhusu Syria Lakhdar Brahimi.Picha: Reuters/Khaled al-Hariri

Ban anapendelea Iran ishiriki mazungumzo hayo,lakini waziri Kerry alisisitiza msimamo wa Marekani siku ya Jumapili, huku akiongeza kuwa Iran inaweza kuwa na jukumu la kandoni. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Marie Harf, alirejea msimamo huo jana Jumatatu, akisema kwamba Iran lazima ikubaliane na tamko la Juni 2012 kabla ya kuruhusiwa kuhudhuria mkutano huo.

Uturuki yataka kuondolewa kwa Assad
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema mkutano huo wa amani unapaswa kujielekeza katika kumuondoa Rais Bashar al-Assad madarakani kutokana na kuhusika kwake na vifo vya maelfu ya raia. Erdgogan ameyasema hayo akiwa mjini Tokyo, Japan alikokwenda kwa ziara ya siku tatu yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara.

Wakati hayo yakijiri, wanaharakati ndani ya Syria wameripoti kuwa ndege za serikali zimewauwa raia 10 katika mji wa Bzaa, unaoshikiliwa na waasi kaskazini mwa nchi hiyo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,afpe
Mhariri: Mohamed Khelef