1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran huenda ikawekewa tena vikwazo vya kimataifa

Yusra Buwayhid
13 Novemba 2019

Kitisho cha nchi za Ulaya cha kutaka kuirejeshea Iran vikwazo vya Umoja wa Mataifa, ni ishara ya kukosekana kwa maelewano ya kidiplomasia katika harakati za kutaka kuyaokoa makubaliano ya kinyuklia ya mwaka 2015.

https://p.dw.com/p/3Swk9
Iran IR 6 Zentrifugen
Picha: picture-alliance/AP Photo/IRIB

Tangu Marekani kujitoa katika makubaliano hayo, Uingereza, Ufaransa pamoja na Ujerumani zimekuwa zikijaribu kuyaokoa makubaliano hayo. Huku Iran kwa upande wake ikiahidi kupunguza kiwango cha mpango wake wa urutubishaji wa madini ya Urani. Badala yake Iran ilitaka ilindwe na vikazo vya kiuchumi vinavyoumiza uchumi wake.

Lakini mataifa hayo matatu ya Ulaya hazikuweza kutimiza ahadi hiyo. Kwavile zimeshindwa kuilinda Iran na vikwazo vipya vya Marekani, ambavyo vimezorotesha biashara yake muhimu ya mafuta. Hivyo Iran nayo imeanza kuvunja ahadi zake chini ya makubaliano hayo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya atomiki (IAEA), limethibitisha hivi karibuni kwamba Iran imeanza tena kurutubisha madini ya urani katika kinu chake cha chini ya ardhi cha Fordow. Huku ikitumia mashine za hali ya juu, ambazo zimepigwa marufuku chini ya makubaliano hayo.

Urutubishaji wa madini ya urani ni njia muhimu ya kutengeneza mafuta ya kuripua bomu la atomiki. Iran hata hivyo imesafisha madini hayo kwa asilimia 4.5, kiwango ambacho kinatumika kuzalisha tu umeme. Kutengeneza bomu la atomiki madini hayo yanahitaji kusafishwa katika kiwango cha asilimia 90.

Licha ya hayo, hatua hiyo imezishtua nchi hizo za Ulaya, ambazo awali zilikuwa zikitupilia mbali taarifa za Iran kukiuka makubaliano ya nyuklia.

Iran Atomprogramm
Fundi wa mitambo ya kurutubisha madini ya urani nchini IranPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Salemi,

Kwa mara ya kwanza hivi karibuni, Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani zimetishia kuiwekea tena Iran vikwazo vya kimataifa. Kufuatia mkutano wa mawaziri wake wa mambo ya nje uliofanyika mjini Paris, Ufaransa, mawaziri hao wamesema wako tayari kutumia utaratibu wowote ule wa kutatua mgogoro huo kuhusu makubaliano yao.

Kura ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Chini ya masharti ya mpango wa 2015, ikiwa upande wowote unaamini upande mwengine hautimizi ahadi zake, wanaweza kuwasilisha lalamiko katika Tume ya Pamoja inayojumuisha Iran, Urusi, China, nchi hizo tatu za Ulaya, pamoja na Umoja wa Ulaya.

Iwapo upande unaolalamika hautopata suluhisho kupitia tume hiyo, basi lazima uliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo litalazimika kuitisha kura kati ya siku 30 juu ya azimio la kuendelea kuiwekea Iran vikwazo.

Mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya amesema kwa upande wao hawataki kujitoa katika makubaliano hayo mapema mno. Lakini pia hawaweza kutochukua hatua yoyote. Ameongeza kwamba Urusi na China hawatochukua hatua, lakini Ulaya lazima ionyeshe msimamo wake.

Wanadiplomasia wamesema mkutano wa pande mbili juu ya makubaliano hayo ya nyuklia utafanyika wiki ijayo kujadili maendeleo ya hivi karibuni. Wameongeza kwamba nchi za Ulaya hazitofanya maamuzi ya mwisho kabla ya Januari, wakati Iran inapotarajiwa kutangaza duru ya pili ya hatua za kujiweka mbali na makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amerejea tena matamshi yake kwamba Iran nayo imewasilisha malalamiko, na imesita kutimiza ahadi zake za makubaliano ya nyuklia kwa sababu nchi za Ulaya zimeshindwa kuilinda na vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa na Marekani.

rtre