Guterres ampongeza Mohammadi kwa kushinda Tuzo ya Nobeli
6 Oktoba 2023Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, amesema tuzo hiyo ni heshima kwa wanawake wote wanaopigania haki zao hata wanapoweka afya na maisha yao hatarini.
Kupitia taarifa, Guterres amesema kuchaguliwa kwa Mohammadi ni ukumbusho muhimu kwamba haki za wanawake na wasichana zinarudishwa nyuma ikiwemo kupitia mateso ya watetezi wa haki za binadamu nchini Iran na kwingineko. Umoja wa Mataifa umeitolea wito Iran kumuachilia huru Mohammadi kutoka jela.
Naye Narges Mohammadi mwenyewe amesema kupitia taarifa aliyoitumia gazeti la New York Times kwamba msaada wa kimataifa anaoupata na kutambuliwa kwa utetezi wake wa haki kunampa nguvu, wajibu, ari na pia matumaini zaidi. Ni kulingana na chapisho kwenye mtandao wa X.
Mohammadi ambaye bado yuko jela amesema anatumai ushindi huo utawafanya Wairan wanaoandamana kushinikiza mabadiliko, kuwa na nguvu zaidi na kwamba ushindi uko karibu.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemsifu pia mshindi huyo na kuitaja tuzo hiyo "chaguo bora kwa mpigania haki ambaye kila wakati alikabiliana na hali halisi, ukweli, ukatili wa utawala wa sasa, ikiwa ni pamoja na mateso anayoyapata jela kwa miaka kadhaa pamoja na hukumu za kutisha.