Iran itafanya mazungumzo na Marekani ikiondolewa vikwazo
6 Agosti 2019Baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje, Mohammad Zarif, Rouhani amesema vita na Iran ndiyo mama wa vita vyote na pia amani na nchi hiyo ndiyo mama wa amani. Halikadhalika Rouhani amesema kuwa Iran itakubali kufanya mazungumzo hayo hata kama Marekani haitorudi katika makubaliano ya nyuklia yaliyoafikiwa mwaka 2015.
"Jamhuri ya Kiislamu ya Irani inataka kufanya mazungumzo, na ikiwa Marekani nayo kweli inataka kuzungumza, basi lazima kwanza ituondolee vikwazo. Kurudi au kutorudi kwenye makubaliano ya nyuklia ni uamuzi wao wenyewe na sisi hatujali," amesema Hassan Rouhani.
Rais huyo wa Iran ameongeza kuwa lazima Marekani iondoe vikwazo vyote ili isiwe inatenda makosa ya jinai dhidi ya haki za binadamu. Amelleza kuwa Iran haitoweza kufanya majadiliano na muuaji.
Mivutano kati ya Iran na Marekani ilianza kuzuka baada ya Trump kuiondoa Marekani kutoka katika makubaliano ya nyuklia mnamo Mei 2018, na kuiwekea Iran vikwazo vikali dhidi ya sekta zake za mafuta na benki, kama sehemu ya kampeni yake ya kutaka kuiongezea shinikizo ili nchi hiyo ikubali vile inavyotaka Marekani.
Iran yagoma kutimiza masharti ya kinyuklia
Mwaka mmoja baadae Iran ilianza kulipiza kisasi kwa kutotimiza baadhi ya masharti ya makubaliano hayo ya nyuklia ambayo yalijumuisha mataifa mengine yenye nguvu, Uingereza, Ufaransa, China, Urusi na Ujerumani.
Wiki iliyopita serikali ya Trump pia ilitangaza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zarif. Na mwezi uliopita Trump alitangaza kumuwekea vikwazo sawa na hivyo kiongozi wa kidini wa Iran Ayatollah Khamenei
Soma zaidi: Marekani yamuwekea vikwazo waziri wa mambo ya nje wa Iran
Iran pia imekuwa katika mzozo mwengine na Marekani pamoja na mshirika wake Uingereza kufuatia wanajeshi wa jeshi la majini wa Uingereza kuikamata meli kubwa ya mafuta ya Iran katika eneo la Gibraltar mnamo Julai 4.
Wiki kadhaa baadae, Walinzi wa Mapinduzi ya Iran waliikamata pia meli ya kusafirishia mafuta ya Uingereza katika Mlango Bahari wa Hormuz - njia muhimu inayotumika kusafirisha humusi ya mafuta duniani kote.
Rouhani pia ameongeza kwamba haiwezekani Iran ikawa haina ruhusa kupita katika Mlango wa Bahari wa Gibraltar, lakini nchi za Magharibi zikawa zina uhuru wa kutumia Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Chanzo: ap,rtre,afp