1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaandaa uchaguzi wa rais

18 Juni 2021

Wapiga kura nchini Iran leo Ijumaa wanapiga kura kumchagua rais mpya huku mahudhurio yakihofiwa kuwa ya chini kutokana na hali ngumu ya kimaisha iliyochochewa na vikwazo vya mataifa ya Magharibi.

https://p.dw.com/p/3v9SD
Iran Wahlen
Picha: Fatemeh Bahrami/AA/picture alliance

Vituo vya kura nchini humo vilifunguliwa saa moja asubuhi kwa zoezi hilo la kupiga kura ambalo limepuuzwa na watu wengi baada ya jopo lililo chini ya kiongozi wa juu kabisa nchini humo Ayatollah Ali Khamenei kuwazuia mamia ya wagombea, pamoja na wanamageuzi na washirika wa Rouhani kushiriki katika kinyang'anyiro hicho. Hatua hiyo imewafanya wachambuzi nchini humo kuamini kuwa Ebrahim Rais ndiye anayetarajiwa kuchukuwa uongozi wa taifa hilo huku mshindani wa pekee anayewakilisha upande wa Rouhani, Abdolnasser Hemmati, aliyekuwa mkuu wa benki kuu nchini humo akisema kuwa washindani wengine katika kinyang'anyiro hicho ni kama vibaraka wa Raisi.

Khamenei awahimiza wananchi kupiga kura

Ayatullah Khamenei alipiga kura yake mjini Tehran, ambapo aliwahimiza wananchi kushiriki katika kura hiyo kwa wingi. Televisheni ya taifa ilionesha milolongo mirefu nje ya vituo hivyo vya kura katika miji mbali mbali. Zaidi ya raia milioni 59 nchini humo wanastahiki ya kupiga kura. Vituo hivyo vitafungwa mwendo wa saa moja na nusu usiku lakini muda huo unaweza kuongezwa kwa masaa mawili huku matokeo yakitarajiwa kutolewa kufikia mchana hapo kesho Jumamosi.

Iran Wahlen
Ebrahim Raisi- Mgombea urais Picha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance

Huku kukiwa na hali isiyokuwa wazi ya juhudi za Iran kufufua mkataba wake wa nyuklia wa mwaka 2015 na ongezeko la umaskini nchini humo baada ya miaka kadhaa ya vikwazo vya Marekani, kura ya mara hii inaonekana kama kura ya maamuzi kuhusu jinsi utawala wa nchi hiyo unavyoshughulikia mizozo mbali mbali.

Ushindi wa Raisi utathibitisha kumalizika kisiasa kwa wanasiasa wa msimamo wa wastani kama Rouhani, aliyedhoofishwa na uamuzi wa Marekani wa kujiondoa katika mkataba wa nyuklia na kurejesha vikwazo kwa nchi hiyo katika hatua ambayo ilizuia kuwepo kwa uhusiano wa karibu na mataifa ya Magharibi. Iwapo atachaguliwa, Raisi atakuwa rais wa kwanza wa Iran anayehudumu kuwekewa vikwazo na Marekani hata kabla ya kuingia ofisini kutokana na kuhusika kwake na hukumu za vifo kwa wafungwa wengi wa kisiasa mnamo mwaka 1988 pamoja na wakati wa kuhudumu kwake kama mkuu wa mahakama ya Iran inayoshtumiwa vikali kimataifa kwa kutoa hukumu hizo.