1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaanza kusaka mrithi wa Ahmadnejad

7 Mei 2013

Zoezi la kuwasajili wagombea wa urais tarehe 14 Juni mwaka huu nchini Iran limeanza siku ya Jumanne, ambapo wahafidhina kadhaa wameonyesha nia ya kugombea nafasi hiyo, lakini wanamageuzi muhimu bado hawajajitokeza.

https://p.dw.com/p/18TWV
Rais wa Iran Mahmoud Ahmadnejad
Rais wa Iran Mahmoud AhmadnejadPicha: picture-alliance/dpa

Wizara ya mambo ya ndani ya Iran ilianza kuwasajili wagombea asubuhi ya Jumanne, huku waziri wa wizara hiyo Mostafa Mohammed Najjar akiwashauri wale wote walio na nia ya kugombea kutosubiri hadi hadi siku ya mwisho ili kujiandikisha, na wakati huo huo akionya dhidi ya kuanza kampeni mapema. Uchaguzi wa Iran utafuatiliwa kwa karibu zaidi na nchi za magharibi, miaka minne baada ushindi wa Mahmoud Ahmedinejad kwa muhula wa pili kusababisha maandamano ya vurugu yaliyokandamizwa na serikali kwa nguvu ya kutisha.

Kiongozi wa juu kabisaa nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei.
Kiongozi wa juu kabisaa nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei.Picha: picture-alliance/dpa

Katiba yamzuia Ahmadnejad kugombea tena

Chini ya katiba ya Iran, rais Ahmadinejad hawezi kugombea tena kwa muhula wa tatu mfululizo. Mrithi wake atakabiliana na changamoto kadhaa, ikiwemo uchumi wa Iran unaodhoofishwa na vikwazo vya kimataifa, vinavyolenga kushinikiza nchi hiyo kuachana na mpango wake wa nyuklia. Mchakato wa kuwachuja wagombea umekabidhiwa kwa Baraza la Wasimamizi lisilo la kuchaguliwa, na linalodhibitiwa na wahafidhina walioteuliwa na kiongozi wa juu kabisa wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ambae ndie mwenye kauli ya mwisho katika mambo yote muhimu nchini humo.

Baraza hilo linatarajiwa kutangaza majina ya wale watakaoidhinishwa kugombea ifikikapo tarehe 23 Mei. Wahafidhina wengi wameonyesha nia ya kugombea katika uchaguzi huo. Miongoni mwao ni vigogo kama Ali Akbar Velayati, ambaye alikuwa waziri wa mambo ya kigeni kati ya mwaka 1981 hadi 1997, na ambaye kwa sasa ni mshauri wa mambo ya kigeni wa Khamenei -- na Mohammad Baqer Qalibaf, mkuu wa zamani wa polisi, ambaye kwa sasa ni Meya wa jiji la Tehran.

Ahmadinejad anatarajiwa kumsimamisha msaidizi wake wa karibu na mtata, Estandiar Rahim Mashaie katika uchaguzi huo. Lakini Mashaie, mkurugenzi wa zamani wa shughuli za Ikulu, amekuwa akilaumiwa na wahafidhina wenye msimamo mkali kutokana na mawazo yake ya kizalendo na kiliberali ambayo wanayachukulia kuwa ni upotofu.

Aliekuwa mpinzani mkuu wa Ahmanejad katika uchaguzi wa mwaka 2009, Mir Houssein Mousavi, ambae kwa sasa yuko katika kifungo cha nyumbani.
Aliekuwa mpinzani mkuu wa Ahmanejad katika uchaguzi wa mwaka 2009, Mir Houssein Mousavi, ambae kwa sasa yuko katika kifungo cha nyumbani.Picha: AP

Wanamageuzi bado kutoa mgombea

Kwa upande mwingine, wanamageuzi wanaodharauliwa bado hawajatoa mgombea mwenye nguvu. Hata hivyo magazeti yanayoegemea siasa za mageuzi na watu muhimu katika nyanja hiyo wamezidisha wito kwa rais wa zamani Mohammad Khatami kujiunga katika kinyanganyiro hicho. Wito huo unarudia ule uliyotolewa na mtangulizi wa Khatami, mhafidhina mwenye msimamo wa wastani, Akbar Hashemi Rafsanjani.

Wiki iliyopita waziri wa upelelezi Heydar Moslehi aliwaonya marais hao wawili wastaafu kuhusiana na ushiriki wao katika vuguvugu la maandamano yaliyofuatia uchaguzi wa mwaka 2009 ambao matokeo yake yalipingwa. Maelfu ya watu waliingia mitaani na kuandamana baada kuchaguliwa tena kwa Ahmadnejad, baada ya wagombea wa upande unaopendelea mageuzi, Mir Hossein Mousavi na Mehdi Karroubi kudai kuwepo na udanganyifu mkubwa.

Maandamano hayo yalipelekea ukandamizaji wa kiwango cha juu kutoka kwa vyombo vya dola, na hadi wakati huu, wanamageuzi wamenyamanzishwa. Mousavi na Karroubi wamewekwa katika kifungo cha nyumbani kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Zoezi la kuchuja linalofanywa na baraza la wasimamizi linaendeshwa kwa kuzingatia vifungu vya katiba, ambavyo vinawataka wagombea kuwa na historia ya kisiasa na kidini, na kuamini katika kanuni za Taifa la Kiislamu na dini yake rasmi.

Umati wa wafuasi wa Mir Hussein Mousavi wakati wa kampeni za mwaka 2009.
Umati wa wafuasi wa Mir Hussein Mousavi wakati wa kampeni za mwaka 2009.Picha: AP

Yeyote anayetaka kugombea laazima awe na umri usiopungua miaka 18, lakini umri wa mwisho kabisaa laazima uainishwe. Mgombea atayepita katika chujio la baraza atakuwa na wiki tatu za kupiga kampeni, kabla ya uchaguzi hapo Juni 14. Mwaka 2009 jumla ya Wairani 475 walijiandikisha kama wagombea, lakini ni wanne tu waliopita katika mchujo, wakiwemo Mohsen Rezaei, kamanda wa zamani wa vikosi vya kulinda Jamhuri, ambaye anatarajiwa kugombea tena.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman.