Iran yakana kuidungua ndege ya Ukraine
10 Januari 2020Mkuu wa mamlaka ya anga nchini Iran Ali Abedzadeh amesema hii leo kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran kwamba alikuwa na uhakika kwamba ndege hiyo haikudunguliwa na makombora. "Kama nilivyosema kwa kuzingatia sheria kuna ushirikiano kati ya mifumo ya ulinzi wa angani na mamlaka ya safari za anga. Watumishi wetu wa mamlaka ya anga na wa mfumo wa kujilinda angani wanashirikiana bega kwa bega, kwa hiyo haiwezekani kabisa kwa kitu kama hicho kutokea." alisema Abedzadeh.
Ameitaka pia Marekani na Canada kuthibitisha madai hayo.
Aidha Iran imeialika kampuni ya ndege ya Marekani ya Boeing kushiriki kwenye uchunguzi wa ajali hiyo ya ndege ya shirika la ndege la Ukraine iliyosababisha vifo vya watu wote 176 waliokuwa kwenye ndege hiyo.
Ni hatua inayofuatia tamko la viongozi wa mataifa ya magharibi kwamba ndege hiyo ilidunguliwa na makombora ya Iran ya kutokea ardhini bila ya kukusudia, masaa kadhaa baada ya Iran kushambulia kwa makombora makambi ya Marekani yaliyoko Iraq ili kulipiza kisasi cha mauaji ya kiongozi wa vikosi vya Qurds Qassem Soleimani kwenye shambulizi la Marekani mjini Baghdad.
Msemaji wa baraza la mawaziri la Iran Ali Rabiel pia amefutilia mbali uwezekano wa madai hayo ya magharibi akiyaelezea kama kutia chumvi kwenye kidonda kinachouma kwa familia za wahanga wa ajali hiyo.
Rais wa Ukraine Volodymir Zelenskiy amesema atazungumza baadae hii leo na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo kuhusu madai hayo. Zelensky ameandika kwenye ukurasa wa Facebook kwamba ingawa hawawezi kuondoa uwezekano wa kudunguliwa ndege hiyo, lakini hilo bado halijathibitishwa. Amesema lengo lao ni kudhihirisha ukweli usiopingika kwa kuwa thamani ya mwanadamu iko juu ya matamanio ya kisiasa.
Ufaransa kupitia waziri wa mambo ya nje Jean-Yves Le Drian imesema hii leo iko tayari kushiriki kwenye uchunguzi huo kwa kutoa wataalamu, ikisema kuna umuhimu wa ukweli kujulikana. Waziri mkuu wa Sweden Stefan Lovren naye ametaka kufanyika uchunguzi wa kina na wa wazi kuhusu madai hayo.