Iran yalaani vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi yake
15 Oktoba 2024Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ismaeil Baghaei, amesema hayo leo, siku moja baada ya Umoja wa Ulaya kuiwekea Iran vikwazo.
Jana Umoja wa Ulaya ulikubaliana kuweka vikwazo kwa watu saba na kampuni saba, likiwemo shirika la ndege la Iran, kutokana na kuhusika kupeleka makombora ya Iran nchini Urusi.
Soma pia: Mawaziri wa EU wagawika kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amethibitisha kuwekwa kwa vikwazo hivyo.
"Na leo Baraza la Umoja wa Ulaya, limepitisha vikwazo kutokana na Iran kupeleka makombora Urusi. Hivi ni vikwazo vya kwanza dhidi ya Iran kwa kupeleka makombora.''
Mwezi uliopita, Marekani, kwa kuzingatia taarifa zake za kijasusi, ilisema Urusi ilipokea makombora kutoka kwa Iran kwa ajili ya kutumika katika vita vya Ukraine.
Hata hivyo, Baghaei amekanusha madai kuwa nchi yake iliipatia Urusi makombora.