1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaonya hujuma zinaathiri mazungumzo ya Vienna

13 Aprili 2021

Iran imeonya kuwa vitendo vya hujuma na vikwazo havitaipa Marekani uwezo wa nguvu ya ushawishi wa ziada katika mazungumzo ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015. Iran pia imeituhumu Israel kwa kuihujumu.

https://p.dw.com/p/3rvg8
Iran Sergej Lawrow in Teheran
Picha: Russian Foreign Ministry Press Service/AP/picture alliance

Matamshi hayo ya Mohammad Javad Zarif aliyoyatoa wakati wa ziara ya mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov, yamekuja wakati Marekani ikisisitiza kwamba haikuhusika kwa vyovyote na hujuma ya Jumapili dhidi ya kinu cha nyuklia cha Natanz.

Zarifa alisema mjini Tehran Wamarekani wanapaswa kufahamu kwamba siyo vikwazo wala vitendo vya hujuma vitawapa nyenzo kwa ajili ya mazungumzo, na kuongezeka kuwa wanapaswa kujua kwamba vitendo hivyo vitaifanya tu hali kuwa mbaya kwao.

Iran Urananreicherungsanlage in Natanz
Mashine pewa za urutubishaji wa urani zilizopo katika kiwanda cha nyuklia cha Natanz.Picha: AEOI/ZUMA Wire/imago images

Msemaji wa ikulu ya White House Jen Psaki aliwaambia waandishi habari kwamba Marekani haikuhusika kwa namna yoyote, na kuongeza kuwa "hatuna cha kuongeza juu ya uvumi kuhusu visababishi."

Soma pia:Iran yadai kushambuliwa kimtandao na Israel 

Wakati haijadai kuhusika, Israel inaaminika pakubwa kuhusika na shambulio hilo lililosabbisha uharibifu wa mashine pewa. Nchi hiyo inapinga vikali makubaliano ya mwaka 2015 na imeapa kuizuwia Iran kutengeneza bomu la atomiki - lengo ambalo Iran imekanusha siku zote kutaka kulifikia.

Awali Iran iliripoti kukatika kwa umeme kwenye kiwanda cha Natanz siku ya Jumapili, siku moja baada ya kutangaza kwamba imewasha mashine pewa za kisasa za urutubishaji wa urani, ambazo zilipigwa marufuku chini ya makubaliano hayo.

Urusi yasema yafuatilia matukio kwa karibu

Duru za vyombo vya habari nchini Israel zililihusisha shambulio hilo na idara za usalama za Israel kufanya operesheni ya mtandaoni. Gazeti la New York Times la Marekani, likiwanukuu maafisa wa upelelezi wa Marekani na Israel, pia lilisema kulikuwepo na ushiriki wa Israel katika shambulio hilo, ambalo liliharibu mifumo ya umeme kwenye mashine pewa za chini ya ardhi.

Iran I Atomkraft I Atomanlage Natanz
Muonekano jumla wa kiwanda cha nyuklia cha Natanz, kilomita 270 kusini mwa Tehran.Picha: Getty Images/AFP/H. Fahimi

Urusi ilisema inafuatilia matukio hayo kwa karibu, na kwamba iwapo itathibitishwa kuwa vitendo cha hujuma za mtu vilihusika na tukio hilo, basi dhamira kama hiyo inapaswa kulaaniwa vikali.

Soma pia: Iran yakiri kituo cha Natanz kimeharibiwa kwa moto

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov, pia amesema wana matumaini ya kuyaokoa makubaliano ya nyuklia, na hatimaye kuirejesha Marekani katika makubaliano hayo.

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump aliiondoa nchi hiyo kwenye makubaliano mwaka 2018, lakini utawala mpya wa Joe Biden umeonyesha dhamira ya kurudi kwenye makubaliano hayo yaliofikiwa wakati wa utawala wa Barack Obama, ambapo Biden alikuwa makamu wa rais.

Chanzo: Mashirika