1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yataka mazungumzo ya amani ya Yemen

Admin.WagnerD9 Aprili 2015

Iran imetoa wito kwa Saudi Arabia na washirika wake kutatua mgogoro wa Yemen kwa njia ya kidiplomasia huku Marekani ikisema haiwezi kukivumilia kitendo cha Iran cha kusaidia waasi wa Kishia.

https://p.dw.com/p/1F5GI
Sanaa Jemen Luftangriff Saudi Arabien
Mashambulizi ya angani ya Saudi Arabia na washiriki wake baada ya kuvumilishwa mjini SanaaPicha: Reuters/Khaled Abdullah

Rais Hassan Rouhani wa Iran ametoa wito wa kufikishwa mwisho kwa mashambulizi ya angani yanayofanywa na Saudi Arabia na washirika wake wa mataifa ya Kiarabu, kwa kusema hayawezi kufanikiwa na hivyo kuyataka mataifa katika kanda hiyo kutafuta suluhu kwa mwelekeo kisiasa.

Katika hotuba yake kupitia televisheni rais Rouhani alisema kwa mtazamo wake taifa kama Yemen haliwezi kusalimu amri kwa sababu ya mabomu na kuongeza kwamba wote waje pamoja na kufikiria namna ya kumaliza vita. Wanapaswa kufikiri kuhusu kusitishwa mapigano.

Wiki mbili za mashambulizi

Saudi Arabia na muungano wa majeshi wenye kujumuisha mataifa ya Ghuba ya Uarabuni yameendesha mashambulizi ya angani dhidi ya harakati za Houthi katika kipindi cha takribani wiki mbili kwa lengo la kuwaondoa wapiganaji hao katika mji wa kusini wa Aden.

Jemen Flüchtlinge Sanaa
Baadhi ya raia wakiukimbia mji wa SanaaPicha: Reuters/K. Abdullah

Muungano huo unasema unamuunga mkono rais wa Yemen Abdi-Rabbu Mansour Hadi dhidi ya jaribio la mapinduzi la Houthi na vilevile kuituhumu Iran kwa kulipa silaha kundi hilo, madai ambayo yamekanushwa na taifa hilo linalofuata madhehebu ya Kiislamu ya Shia.

Marekani yaionya Irani

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry amesema taifa lake haliwezi kujiweka kando wakati Iran ikiwasaidia waasi wa Kishia ambao wameyateka maeneo mengi ya Yemen. Waziri Kerry alikiambia kituo cha televisheni cha PBS kwamba wamebaini kuwa kila baada ya wiki kumekuwa na ndege za Iran zinazotua katika ardhi ya Yemen.

Lausanne Atomverhandlungen Abschlußstatement Kerry
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Jonh KerryPicha: Reuters/Ruben Sprich

Kutokana na kitendo hicho amesema Iran lazima itambue kwamba Marekani haiwezi kukaa kimya wakati hali ya utulivu ikivurugwa katika kanda hiyo.

Marekani inaunga mkono muungano wa mataifa yenye idadi kubwa ya Waislamu wa Madhehebu ya Sunni, wenye kuongozwa na Saudi Arabia, ambao unaendesha kampeni ya mashambulizi ya angani katika jitihada zake za kumrejesha madarakani Rais Abdi-Rabbu Mansour Hadi wa Yemen ambae amelazimishwa kulikimbia taifa lake.

Waasi 20 wauwawa katika mapigano

Na katika uwanja wa mapambano kiasi ya waasi 20 wa Houthi wameuwawa huko kusini mwa Yemen, kufuatia mashambulizi ya anga ya muungano unaongozwa na Saudi Arabia pamoja na kukabiliwa vikali na wapiganaji wanaounga mkono serikali. Chanzo kimoja kutoka kwa wapiganaji hao kilisema wapiganaji 14 wa Houthi waliuwawa katika mashambulizi hayo karibu na wilaya ya Dar Saad, iliyopo kusini mwa Aden. Na wengine sita wameuliwa na wanapiganaji watiifu kwa serikali katika karibu na mji wa Daleh.

Waasi wa Houthi wamefanikiwa kudhibiti sehemu kubwa ya Yemen, ikiwemo mji mkuu wa Sanaa, na kuungana na wapiganaji watiifu kwa mtawala wa zamani wa muda mrefu wa taifa hilo Ali Abdullah Saleh, ambae alilazimishwa kuondoka madarakani mwaka 2012 baada ya mwaka mmoja tangu kuanza kwa vuguvugu la mataifa ya Kiarabu.

Mwandishi: Sudi Mnette AFP RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga