1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatangaza hatua mpya za kukiuka makubaliano ya nyuklia

4 Novemba 2019

Mkuu wa shirika la nishati ya Atomiki nchini Iran Ali Akbar Salehi, amesema nchi hiyo imechukua hatua nyengine ya kukiuka makubaliano ya mkataba wake wa nyuklia uliotiwa saini mwaka 2015

https://p.dw.com/p/3SRkD
Ali Akbar Salehi
Picha: mehr

Mkuu huyo wa shirika la nishati ya Atomiki nchini Iran Ali Akbar Salehi, amesema hii leo wamezindua  mitambo aina ya 30 IR-6 na kwa sasa taifa hilo lina mitambo  60 ya kisasa hali inayoonesha upeo na azma yao.

Iran imeiita hatua hiyo kuwa majibu ya moja kwa moja kwa rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia yaliotiwa saini mwaka 2015. Ali Akbar Salehi amesema Iran iliyokuwa inazalisha gramu 450 sawa na pauni moja ya madini ya Urani kwa siku, sasa itakuwa inazalisha kilo 5 ambayo ni sawa na pauni 11 kwa siku.

Tangazo hilo linalojumuisha Iran pia kutangaza mitambo inayofanya kazi kwa kasi ya mara 50 kuliko ile ilizokubaliwa katika makubaliano hayo, limekuja wakati waandamanaji nchini humo wakiadhimisha kumbukumbu ya miaka 40 tangu wanafunzi wakiiran walipouteka ubalozi wa Marekani mjini Tehran hali iliyoanzisha mgogoro wa siku 444. 

Kwa kuanzisha mitambo yenye  nguvu kubwa ya urutubishaji madini ya urani , wanaharakati wanakadiria kuwa Iran itachukua chini ya mwaka mmoja kuwa na vifaa vyote vinavyohitajika kuunda silaha za nyuklia, iwapo itaamua kufanya hivyo.

Iran mara kwa mara imekuwa ikisisitiza kuwa operesheni zake ni kwaajili ya amani, japokuwa jamii ya Kimataifa inahofia shughuli za taifa hilo, hali iliyosababisha kuwepo makubaliano hayo ya nyuklia yaliotiwa saini mwaka 2015 ili taifa hilo lidhibiti urutubishaji wa madini yake ili iondolewe vikwazo vya kiuchumi ilivyoekewa.

Hassan Rouhani anatarajiwa kutanga hatua zaidi za kukiuka makubaliano

Iran l Teilausstieg aus dem Atomabkommen l Besuch des Kernkraftwerks Buschehr - Rouhani
Rais wa Iran Hassan Rouhani akiwa na Mkuu wa shirika la nishati ya Atomiki Ali Akbar Salehi,Picha: picture alliance/AP/Iranian Presidency Office/M.Berno

Kwa sasa Iran inarutubisha madini kwa asilima  4.5 ambayo inakiuka makubaliano yanayoruhusu madini kurutubishwa kwa kiwango kisichozidi asilimia 3.67 ambayo ndio inayohitajika kwa shughuli za amani na ikiwa ni asilimia chache sana kwa kiwango kinachohitajika kutengeneza silaha za nyuklia.

Huku hayo yakiarifiwa,  msemaji wa serikali ya Jamhuri hiyo ya kiislamu  Ali Rabiei amesema rais Hassan Rouhani anatarajiwa kutangaza hatua nyengine zaidi za kukiuka makubaliano hayo.

Hata hivyo shirika la kimataifa  la kudhibiti silaha za nyuklia IAEA bado mpaka sasa halijatoa tamko lolote juu ya uamuzi huo wa Iran huku Umoja wa Ulaya ukisema bado unashikilia makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 licha ya rais Trump kuiondoa Marekani katika makubaliano hayo.

Maja Kocijancic, msemaji wa halmshauri ya Umoja wa Ulaya amesema, makubaliano hayo bado ni suala la usalama sio tu kwa eneo hilo au ulaya bali kwa dunia nzima, huku akisema kujitolea kwa Umoja wa Ulaya katika makubaliano hayo kunatokana na utekelezwaji wake kikamilifu na Iran.

ap,reuters.afp