Iraq na Uturuki wafanya mazoezi ya pamoja kijeshi
27 Septemba 2017Iraqi na Uturuki zimefanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi hapo jana huku waziri mkuu wa Iraq Haider al- Abadi akiwataka viongozi wa jimbo hilo lenye utawala wa ndani kukabidhi viwanja vyao viwili vya kimataifa vya ndege chini ya serikali kuu ifikapo Ijumaa au vinginevyo ndege hazitaruhusiwa kutua au kuruka katika viwanja hivyo.
Al-Abadi alitoa sharti hilo ikiwa ni siku moja baada ya kufanyika kura ya maoni katika kuelekea Wakurdi wa Iraqi kuwa na taifa lao na ambayo ameiita ni kosa la kimkakati la kihistoria lililofanywa na uongozi wa wakurdi.
Wakati matokeo ya mwisho ya kura hiyo ya maoni yakiwa bado hayajatangazwa, kiongozi wa wakurdi Masoud Barzani amesema wengi waliopiga kura hiyo ya maoni waliunga mkono uhuru wa jimbo hilo.
Aidha Barzani pia ametaka kuwa na mazungumzo na serikali kuu ya mjini Baghdad ambapo pia aligusia juu ya mustakabali katika kuelekea kupatikana uhuru wa jimbo hillo huku akisisitiza kuwa angependelea kutatua masuala yote na serikali ya Iraq kwa njia ya amani.
Kura ya maoni ni pigo kubwa kwa Marekani
Wakati huohuo kura hiyo ya maoni ya jamii ya wakurdi wachache nchini Iraq yenye nia ya kutaka wawe na taifa lao ni pigo kubwa kwa Marekani ambayo imetumia miaka mingi, mabilioni ya dola pamoja na kugharimu maisha ya wanajeshi katika kujaribu kuiweka Iraq pamoja. Hiyo ikiwa ni pamoja na afisa mmoja wa Marekani pamoja na maafisa wengine wanaohusika na masuala ya sera.
Baadhi ya washirika wa karibu wa Marekani katika mashariki ya kati wamesema njia za kidiplomasia kuwashawishi viongozi wa kikurdi kuzuia kura hiyo ziligonga mwamba hali ambayo inaoneka ni ushahidi mpya unaonesha kupungua kwa nguvu ya ushawishi ya Marekani.
" Hili ni pigo kubwa linazima hoja ya kuwa ni Marekani pekee ambayo inaweza ikaifanya Iraq iwe kitu kimoja " alisema James Jeffrey balozi wazamani wa Marekani nchini Iraq.
Wakurdi ambao wamelitawala jimbo hilo lililo na utawala wake wa ndani nchini Iraq tangu wakati wa uvamizi wa Marekani nchini humo uliopelekea kuondolewa kwa utawala wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Saddam Hussein wanaamini kuwa kufanyika kura hiyo ya maoni ni hatua moja ya kihistoria ya kizazi hicho kuelekea kuwa na taifa lao.
Aidha kura hiyo inawapa nguvu viongozi wa kikurdi kuanzisha mazungumzo ya kudai uhuru wa jimbo lao lenye zaidi ya watu milioni 8.3.
Hatua hiyo pia inaweza kukwamisha juhudi zinazoungwa mkono na Marekani za kuleta uthabiti nchini Iraq pamoja na kulisambaratisha kabisa kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu pamoja na makundi mengine ya aina hiyo.
Wakati huohuo Urusi hii leo imeinya Iraq pamoja na wakurdi dhidi ya kuchukua hatua yoyote ambayo inaweza ikavuruga amani ya Mashariki ya Kati kufuatia kura hiyo ya maoni na kuzitaka pande zote kufanya mazungumzo kwa ajili ya kutafuta suluhisho katika misingi ya kuwa na taifa moja la Iraq.
Kwa upande mwingine Ufaransa kupitia kwa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Jean-Yves le Drian amelionya jimbo la kikurdi nchini Iraq kuwa kujitangazia uhuru wa jimbo hilo kutaliyumbisha jimbo hilo na kutoa mwito kwa serikali ya Iraq kuwapa utawala mkubwa wa ndani.
Mwandishi: Isaac Gamba/dw/rtre
Mhariri : Josephat Charo