1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq: Watu wengi wafa katika maandamano ya kupinga serikali

6 Oktoba 2019

Takriban watu 100 wamepoteza maisha, katika maandamano mapya ya kupinga serikali nchini Iraq. Vifo hivyo, vimetokana na makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.

https://p.dw.com/p/3QmrT
Irak Anti-Regierungsproteste | Ausschreitungen & Gewalt in Bagdad
Picha: Reuters/W. al-Okili

Tangu siku ya Jumanne, maelfu ya watu wameingia mabarabarani nchini humo na kuandamana kupinga rushwa, ukosefu wa ajira, maji safi na huduma mbovu hasa za umeme. Watu wanne walikufa kwenye maandamano hayo hapo jana Jumamosi wakati maafisa wa usalama walipowafyatulia waandamanaji wapatao 200 waliokuwa wamekusanyika katika mji mkuu Baghdad.

Maandamano ya Iraq ambayo kwa kiasi kikubwa yanaongozwa na vijana yaliibuka tena mwishoni mwa wiki baada ya amri ya kutotoka nje kuondolewa mjini Baghdad, mapema siku ya Jumamosi. Tume ya Haki za Binadamu ya Iraq imesema karibu watu 4,000 walijeruhiwa katika mapambano ya siku nne kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.

Waziri Mkuu wa Iraq Adil Abdul Mahdi
Waziri Mkuu wa Iraq Adil Abdul Mahdi Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Ozbilici

Mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Irak Jeanine Hennis-Plasschaert, amesema amesikitishwa mno na kulaani vurugu hizo. Hennis-Plasschaert ametoa wito kwa pande zote kutafakari na kuhakikisha kuwa wale waliosababisha vurugu hizo wanachukuliwa hatua za kisheria.

Maandamano hayo iliyoanza siku ya Jumanne yamewashangaza viongozi wa Iraq. Wataalam wanasema hiyo ni changamoto kubwa kwa serikali tangu kuangushwa kwa kundi la wanamgambo wanaojiita Dola la Kiislamu IS miaka miwili iliyopita.

Katika hotuba yake mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu wa Iraq Adel Abdul-Mahdi alisema madai ya waandamanaji kupinga rushwa serikalini ni ya haki. Waziri Mkuu huyo anajaribu kurejesha utulivu baada ya siku kadhaa za vurugu zinazofanywa na wananchi wa Iraq.

Chanzo: /https://p.dw.com/p/3QmIw